Ngome ya Wanawake ya Chama Cha ACT Wazalendo imempinga Rais Magufuli juu ya kauli yake ya dhidi ya watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni kuwa hawapaswi kuendelea na shule, Wanawake wa ACT Wazalendo wanasema kitendo hicho ni kinyume na Katiba
Rais Magufuli wakati akihutubia mkoani Pwani tarehe 22/06/2017 alipiga marufuku wanafunzi wajawazito kuendelea na masomo na kusema kuwa katika serikali yake hawezi kusomesha wazazi hivyo ukijiona umepata mimba ukiwa shule ya msingi au sekondari basi usahau kuendelea na shule.
"Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo inaiona marufuku hiyo kama hatua kali inayomkandamiza na kumbagua mtoto wa kike kwa kumnyima haki yake ya msingi ya kupata elimu. Marufuku hii ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 11(2) inayosema: "Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake". Alisema Esther Kyamba, Katibu, Ngome ya Wanawake
Wanawake wa ACT Wazalendo wanasema kuwa watoto wengi wa vijijini ndiyo wamekuwa wahanga wakubwa wa matatizo ya kupata ujauzito wakiwa mashuleni kutokana na mazingira na miundombinu mibovu inayokuwa ni chanzo cha watoto hao kupata ujauzito.
"Watoto wengi wa kike hasa waishio maeneo ya vijijini ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa matatizo ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kutokana na miundombinu isiyo rafiki ya elimu kama vile ukosefu wa mabweni, kusafiri mwendo mrefu kwenda na kurudi shuleni, kusaidia shughuli za nyumbani na shughuli za kuziingizia kipato familia zao ambapo kote huko hukabiliana na changamoto kadhaa wa kadha zinazoweza kuwasababishia ujauzito. Ngome inaamini ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha inatengeneza mazingira rafiki na salama kwa mtoto wa kike ili nae aweze kupata haki yake ya msingi ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine na sio kumbagua, kumkandamiza na kumnyima haki yake ya elimu" alisema Esther Kyamba