Zitto Afunguka Juu ya Kikao cha Bosi wa Barrick na JPM,,,Adai Hayatakuwa na Tija wala Jipya kwa Taifa..!!!


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) amesema suala la Serikali kukaa na wawekezaji si jawabu la tatizo lililotokea bali kinachotakiwa ni Katiba Mpya yenye kumilikisha utajiri wa nchi kwa wananchi.

Kauli hiyo ya Zitto imekuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kukutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton na kukubaliana kampuni hiyo kufanya mazungumzo na Serikali yake.

Pia Profesa Thornton alisema kampuni yake itakuwa tayari kulipa fedha ambazo Tanzania imepoteza kutokana na uendeshaji wa shughuli zake nchini ikiwa italazimika baada ya majadiliano.

Hatua ya kampuni hiyo kufanya mazungumzo na Rais Magufuli inatokana na taarifa  ya Kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyopewa jukumu la kuchunguza mikataba ya madini na kiwango kilichopo kwenye makanikia yaliyosafirishwa nje na kwenye kontena 277 zilizozuiwa bandarini Dar es Salaam.

Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alipokea taarifa ya Kamati hiyo ambayo ilieleza kuwa Acacia haijasajiliwa na haipo kisheria nchini, jambo ambalo liliibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mengine hususan kwa wanasiasa.

Lakini akizungumza Dar es Salaam jana, Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo alisema chama chake kilihadharisha jambo hilo katika kongamano lake la Rasilimali Madini lililofanyika Juni 3 Dar es Salaam.

“Tulihadharisha hili Juni 3 kwamba mwisho wa siku Serikali itakaa mezani, hivyo tuombe sana hoja za Serikali ziwe na ushahidi wa kutosha, vinginevyo tutaendelea kulia kuibiwa daima,” alisema.

Aliongeza kuwa jawabu la changamoto zilizojitokeza si mazungumzo na wawekezaji, bali ni Katiba mpya yenye kumilikisha utajiri wa nchi kwa wananchi wa Tanzania milele, ambao ndio rasilimali yao.

Juni 3 ACT-Wazalengo ilifanya kongamano la Rasilimali Madini la kujadili nchi inavyonufaika na sekta ya madini ambalo liliibuka na maazimio 10, likiwamo la kutaka mjadala mpana kulinda aina zote za madini nchini.

Watoa mada katika kongamano hilo lililenga kujadili kwa kina sekta hiyo baada ya hivi karibuni Rais John Magufuli kuunda Kamati ya Kuchunguza Mchanga wa Madini unaosafirishwa nje na kutoa ripoti iliyoshitua Taifa.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk Rugemeleza Nshala, Mwenyekiti wa Taasisi ya ONGEA, Dennis Mwendwa na Nico Kajungu wa Numet.

Kamati iliyochunguza mchanga wa madini chini ya uenyekiti wa Profesa Abdulkarim Mruma, ilibaini kuwa kontena 277 zilizozuiwa katika bandari ya Dar es Salaam zina tani 7.8 za dhahabu yenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na Sh trilioni 1.147.

Kiwango hicho kilikuwa tofauti na ambacho Kamati hiyo ilielezwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kwamba kontena hizo zilikuwa na tani 1.1 za dhahabu.

ACT-Wazalendo ilieleza kuwa mbali na kutaka uchunguzi ufanyike kwa madini yote, kongamano hilo lilibaini kuwa takwimu za Kamati zina walakini.

“Takwimu hizi zikikubaliwa kama zilivyo, zitaifanya Tanzania kuwa mzalishaji namba moja wa dhahabu Afrika. Hatuhitaji kupika takwimu au kuongopa, ili kushinda vita vya rasilimali.

“Kunapaswa kuwa na timu huru ya kupitia takwimu zilizotolewa na Kamati ya Profesa Mruma ili kuthibitisha uhalali wake. Kuwa na takwimu sahihi ni muhimu sana kwenye kupata majawabu,” lilieleza azimio la pili.

Azimio lingine ni kwamba katika mapambano ya kulinda rasilimali madini, ni lazima yafanyike mabadiliko ya sheria ya madini na Katiba, ili kufanya madini na maliasili zingine kuwa mali ya wananchi milele.

“Serikali ibadilishe mfumo wa kuchimba madini kwa kuhamia kwenye mfumo wa kugawana mapato ili kuondokana na mfumo wa sasa ambao kimsingi una njia nyingi za kukwepa kodi kwa mbinu halali kabisa,” kilieleza chama hicho katika azimio lake la nne.

Pia kilitaka sauti za wafanyakazi katika migodi ziheshimiwe, haki zao zilindwe na washirikishwe kikamilifu kwenye uamuzi kuhusu sekta ya madini.

“Mikataba ya madini izingatie kuwa kuna uharibifu wa mazingira kwenye uchimbaji madini. Mikataba iwe na vifungu imara vya kulinda mazingira.

“Watu wote walioshiriki kuingia mikataba ya madini na kufanya uamuzi unaolitia Taifa hasara wawajibishwe na kuchukuliwa hatua bila kujali vyeo vyao au lini makosa yalifanyika.”

Katika azimio la nane, kongamano hilo lilipendekeza kufanyika kwa usanifu wa madini ya tanzanite likisema: “Sisi ndio wazalishaji pekee wa tanzanite. Hivyo tuna ukiritimba unaotuwezesha kushawishi kampuni za vito vya tanzanite kujenga viwanda Tanzania.”

Pia lilitaka mikataba yote ya madini ipitiwe upya, kama ikihitajika kurekebishwa ifanyike hivyo ili kulinda maslahi ya umma, kwamba iwapo mikataba husika itabainika kuwa ya hovyo ivunjwe kama ilivyotokea katika nchi za Bolivia, Venezuela, Iran na Botswana.

“Mjadala wa rasilimali madini usiachwe mikononi mwa Serikali ya CCM ambayo ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo sasa,” lilieleza azimio la 10 la kongamano hilo.

“Wananchi wote kupitia asasi za kiraia, vyama vya siasa na umma kwa ujumla washiriki kuhakikisha mjadala juu ya rasilimali madini unafikishwa mwisho kwa maslahi ya umma.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad