Kesi ya madai ya utakatishaji fedha inayowakabili viongozi wa Simba, Rais Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ imetajwa leo Julai 20 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Aveva na Kaburu wanakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka za Klabu ya Simba na kutakatisha dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 650) na wamekuwa rumande tangu Juni 29, mwaka huu.
Aveva peke yake aliweza kufika mahakamani hapo na kushuhudia kesi hiyo ikitajwa huku, Kaburu akishindwa kufika mahakamani kutokana na kudaiwa kuwa ni mgonjwa.
Watuhumiwa wote wamerudishwa rumande baada ya kesi yao kuahirishwa na sasa watarejeshwa mahakamani hapo Julai 31, mwaka huu.
Kabla ya kesi hiyo kutajwa wanachama wa Simba walianza kufika mahakamani mapema ili kujua hatima ya viongozi wao.