Dodoma. Kuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na faini za makosa ya barabarani na mbinu zinazotumiwa na trafiki, kumeibua mjadala kwa wadau wa usafiri na usafirishaji.
Pamoja na mjadala huo, Kamanda wa Trafiki wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Awadh Haji amesema askari wake wataendelea kuvizia barabarani ili kukamata madereva wanaovunja sheria.
Kamanda Awadh ametoa msimamo huo jana alipoulizwa kuhusu ongezeko la kiwango kinachokusanywa kwa makosa ya barabarani na sababu za askari wa usalama barabarani kujificha wakiwa na kamera maalumu wakati wakivizia kukamata madereva wanaoendesha kwa kasi isiyolingana na viwango vilivyopo barabarani.
Mwananchi ilitaka maoni ya wadau mbalimbali wa barabara baada ya Kikosi cha Usalama Barabarani kutangaza ongezeko kubwa la makusanyo ya faini kutoka Sh7.3 bilioni kwa kipindi cha kati ya Januari na Mei mwaka 2016, hadi kufikia Sh12.8 bilioni kwa kipindi kama hicho mwaka huu.
“Kujificha ni mbinu ya medani kufanikisha ukamataji wa madereva wasiotii sheria,” alisema Kamishna Awadh.
“Tutaendelea kufanya hivyo ili kubadilisha tabia zao. Wakiwa na hofu ya kukamatwa, huepuka kufanya makosa.”
Wananchi na wadau wa usafirishaji wamekuwa na maoni tofauti baada ya Kaimu Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya kutoa taarifa ya mapato yaliyokusanywa na trafiki kati ya Januari na Mei mwaka huu kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.
Taarifa hiyo aliyoitoa katikati ya mwezi uliopita ilibainisha kukusanywa kwa Sh12.8 bilioni mwaka huu kutokana na makosa 404,571 zikilinganishwa na Sh7.3 bilioni baada ya makosa 246,695 kukamatwa na askari hao mwaka jana.
Wakati idadi ya makosa ni ongezeko la takriban maradufu, ni ongezeko la theluthi moja tu ya kesi zilizofikishwa mahakamani mwaka huu kulinganisha na mwaka jana.
Mkondya anaamini ufanisi wa kikosi hicho kukabiliana na makosa ya barabarani unaongezeka ikilinganishwa na ongezeko la vyombo vya usafiri vya moto.
Pia, kuwepo kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara dhidi ya makosa yaliyoripotiwa.
“Makosa hayalingani na ongezeko la vyombo vya moto. Kazi kubwa imefanyika,” alisema Mkondya alipozungumza na gazeti hili jana.
Akibainisha ongezeko la changamoto zilizochangia kuongezeka kwa makosa hayo, Awadh alisema licha ya ongezeko la vyombo vya moto barabarani, wakazi wa jiji la Dar pia wameongezeka hivyo kuongeza changamoto za usafiri.
Kutokana na ongezeko la makosa hayo sambamba na faini kubwa zilizotozwa, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alisema kikosi hicho na Jeshi la Polisi kwa ujumla kimejisahau hivyo kuanza kutekeleza majukumu ya taasisi nyingine.
Alisema ongezeko la makosa hayo halipaswi kuwa jambo la kujivunia kwa kuwa linathibitisha kushindwa kwa watendaji waliopewa jukumu hilo ambao wanaona ni rahisi kwao kuongeza makusanyo ya faini, kazi ambayo inatakiwa kufanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Kimsingi aliyetangaza suala hilo alipaswa kujiuzulu kwa sababu amethibitisha kushindwa kukabiliana na changamoto zilizopo,” alisema mbunge huyo maarufu kama Sugu.
Ili kupunguza makosa hayo pamoja na madhara yake kwa jamii ikiwamo vifo vitokanavyo na ajali pamoja na ulemavu wa kudumu, Mbilinyi alilitaka jeshi hilo kuongeza juhudi za kuelimisha madereva badala ya kugeuza makosa kuwa chanzo muhimu cha mapato ya Serikali.
Vilevile alidai askari huwekewa malengo ya makusanyo kwa siku, akisema hata askari hulalamikia suala hilo.
“Tunaokutana nao barabarani wanatuambia tuwasemee. Wakati mwingine wanawabambikia makosa madereva ili kufikia malengo waliyowekewa,” alisema.
Kadhalika alipinga namna tochi zinavyotumika vibaya akieleza kwamba kamera hizo hazitakiwi kufichwa badala yake zitumike hadharani kama ilivyo kwenye mataifa mengine yaliyoendelea.
“Dereva akijua tochi ilipo ataenda mwendo mdogo lakini akishaipita basi atakimbia kufidia muda wake. Hilo halifai nchini kwa wakati huu,” alisema.
Kuhusu kubambikiwa makosa, Jonas Mangula, mkazi wa jijini hapa alisema Machi aligundua leseni yake inatakiwa kurudishwa baada ya pointi zake kumalizika kutokana na makosa lukuki aliyoandikiwa.
Alisema mpaka muda huo, alikuwa amekamatwa mara nne kwa kosa la kuendesha kasi, lakini alikuwa bado hajalipa faini zake. “Nilichanganyikiwa. Kurudisha leseni, maisha yangekuwa magumu hapa mjini,” alisema.
Alisema hata alipojaribu kuomba ushauri kutoka kwa trafiki mmoja, naye alikuwa hajui chochote kuhusu kuisha kwa pointi hizo hivyo akalazimika kwenda kulipa kiasi alichokuwa anadaiwa.
“Nilipolipa tu, makosa yote yalifutika na sasa sidaiwi tena,” alisema Mangula.
Kuhusu makosa hayo, alisema alikuwa anakamatwa akiwa na haraka hivyo kuruhusu aandikiwe: “Wakati mwingine unaona spidi haizidi hata 30 lakini ili kuokoa muda, unapunguza maneno.”
Lamishna Awadh pia alizungumzia hoja ya baadhi ya wadau kwamba makosa hayo yanachangiwa na madereva wanaopewa leseni bila ya kupitia mafunzo, akisema kwa taratibu zilizopo za kupata leseni ni ngumu na yeyote anayebainika hushtakiwa kwa kughushi nyaraka.
“Hatutoi leseni kwa wenye vyeti feki. Shule za udereva huwaleta wahitimu wake wakiwa na magari waliyotumia kuwafunza kwa majaribio. Wanaofuzu pekee ndiyo hupewa leseni. Hata anayekuja mwenyewe, lazima ajaribiwe,” alisema.
Akizungumzia ongezeko la ajali kwa asilimia 60 ndani ya mwaka mmoja, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wasafirishaji Afrika Mashariki (Fearta), Emmanuel Kakuyu alisema usimamizi umeongezeka na kuimarishwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
“Askari wameongezeka barabarani na madereva wanasimamishwa zaidi,” alisema Kakuyu.
Licha ya kuimarika kwa usimamizi unaohusisha doria kama alivyobainisha Awadh, mchumi na mwanaharakati wa kijamii, Profesa Samwel Wangwe alisema ongezeko la mapato hayo huenda likawa limechangiwa na kubadilishwa kwa mfumo wa malipo unaotumiwa na jeshi hilo.
“Madereva wamelipa zaidi kutokana na makosa yao. Mfumo wa kielektroniki unaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye hili,” alisema Profesa huyo.