FLORA Mbasha na Emmanuel Mbasha Watakiwa Kuacha Utoto...Kisa Kizima Hichi Hapa

Hakuna kazi ngumu kama kutoa ushauri kwa watu wenye mgogoro unaohusisha uhusiano wa kimapenzi, kwa sababu ni lazima upande mmoja utachukia, kwani ili kitu kiwe kizuri, ni lazima uwe mkweli kwa asilimia mia moja.

Ni lazima mmoja atachukia kwa sababu siku zote katika uhusiano wa kimapenzi, upande mmoja unakosea.

Barua yangu ya leo inawaelekea kaka na dada yangu, Emmanuel Mbasha na aliyekuwa mkewe, Flora, siku hizi akifahamika kama Madam Flora.

Dada yangu Flora, ninamkubali tangu alipoanza kufanya vyema na Wimbo wa Jipe Moyo, Majaribu na nyinginezo.

Dada Flora, wewe ni mtumishi wa Mungu, kama unaamini kuwa majaribu ni kipimo kwa mtu aliyeokoka, kwa nini unashindwa kumaliza bifu lenu kimya kimya ukizingatia kila mtu kwa sasa ana maisha yake mapya?

Hii ni kwa sababu ya ule unaodaiwa kuwa ujumbe wako kusambaa ambao ulimsema vibaya mumeo wa zamani, kwamba alikuwa chanzo cha kuachana kwenu.

Pengine maisha ya kistaa yamewaathiri au labda huenda bado mnapendana, lakini mbona mnafanya kama hili jambo la kutengana mmelianzisha nyinyi? Nasema hivi kwa sababu migogoro katika ndoa haijaanza leo na wala haitakwisha kesho, ni vitu vya kawaida ambavyo binadamu hupitia.
Sasa kama ilitokea kama ilivyotokea, kuna haja gani ya kupeana vijembe kila kukicha kana kwamba mnashindana kupata tuzo?

Maana kama mmeshindwana na kila mtu ana maisha yake, ya nini kuanza kufukunyua mambo ya faragha kwa watu ambao hawakuwepo huko?

Huko ni kujishushia heshima kwa wote, kwani wewe na mwenzio, mnatambulika kama Watumishi wa Mungu, wapo kondoo wengi ambao walikuwa wanapenda kuiga mfano wenu kama waimbaji na hata wanandoa.

Mmeachana basi, udhaifu na changamoto mlizopitia kwenye ndoa yenu zibaki mioyoni mwenu.
Ndoa yenu imefika mwisho, walimwengu wote wanajua hilo lakini mnapoanza kuchafuana mitandaoni, sidhani kama ni sahihi. Najaribu kuitafuta hekima ya Mungu kati yenu, siioni! Najaribu kujiuliza, mnachafuana kwa sababu ya uwepo wa mitandao ya kijamii au hata kama isingekuwepo mngefanya hivyo?

Kama ni ndoa kuvunjika yenu si ya kwanza, kama ni wanandoa kutibuana na kulumbana, nyinyi si wa kwanza, kama ni migogoro ya kwenye ndoa hata wazazi wetu wameipitia, lakini mbona sababu za mizozo yao hatuijui?

Kinachosikitisha ni kuona kaka Emma naye kaja kujibu mashambulizi kwa maneno makali na yenye vijembe ndani yake. Ingawa hakumtaja mwenzake moja kwa moja, lakini wanaojua fukuto hilo wanajua ndiyo maana vyombo vya habari vimeripoti.

Kaka Emma, mbona ndoa nyingi zina mifarakano mingi sana, mbona wanandoa wengi wameachana lakini wamebaki na vidonda vyao moyoni, si kila jambo la kujibu.

Wakati mwingine ili uonekane una hekima ni vyema ukapotezea tu kuliko kuanza kuandika maneno yanayoondoa hekima, uvumilivu, burasa na utashi wa Kimungu ndani yenu.

Wapo watu wengi ambao wamevunja ndoa zao na kila mtu akawa na maisha yake na wanasalimiana na kupendana kama watu wa kawaida, lakini kwa hiki ninachokiona kwenu si jambo jema, hakuna sababu ya kujengeana uhasama wakati mlioana ili mfurahie maisha lakini kwa kile kilichotokea basi kila mtu afanye yake kwa moyo mweupe.

Vinginevyo ni kama mnatafuta promo ili watu wajue uwepo wenu. Kuna njia nyingi nzuri na zenye mbolea zinazoweza kuwafanya muonekane mbele za watu, kama kufanya kazi yetu na kumtukuza Mungu kupitia nyimbo za Injili au hata kuwapa chochote watoto yatima au watu wenye uhitaji.
Haya mambo mnayofanya waachieni watoto wadogo wa Bongo Fleva wanaoamini kiki ndizo zitawapandisha badala ya kufanya kazi kwa bidii.

GABRIEL NG’OSHA | BARUA NZITO
Maoni & Ushauri:
+255 620 744 592
GPL

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. FLORA NA EMMANUEL ZIGATIENI USHAURI WA MDAU

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad