HOJA Mbili zilivyomtoa TUNDU Lissu Mahabusu Dar


Hakimu Wilbard Mashauri jana alitumia hoja mbili kumpa dhamana, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliyekuwa mahabusu tangu Julai 19 akituhumiwa kwa uchochezi.

“Upendo wa dhati” ulioonyeshwa na jopo la mawakili 18 waliojitokeza kumwakilisha na rekodi yake nzuri, vilitosha kumshawishi hakimu huyo mkazi mkuu kumuachia Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS).

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alikuwa katika hali ya kawaida wakati hakimu Mashauri akisoma uamuzi wake wa pingamizi la dhamana lililowekwa na upande wa mashtaka na baada ya uamuzi huo alitoka nje akitabasamu, akipunga juu mkono wake wa kushoto huku akinyoosha vidole viwili kuashiria nembo ya Chadema.

Katika mkono mwingine alikuwa ameshika chupa ya maji ya kunywa ya lita moja ambayo mwanasheria huyo amewahi kuliambia gazeti hili kuwa huhakikisha anaibeba kila anapokamatwa na polisi kwa ajili ya kuitumia kama mto anapokuwa mahabusu.

Mwanasheria huyo alikuwa amevalia suti ya rangi ya bluu na fulana nyekundu na alisindikizwa na askari wengi kuelekea eneo la kutia saini dhamana kabla ya kumsindikiza hadi kwenye gari lake.

Tofauti na siku nyingine ambazo hupata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari, baada ya kupata dhamana, Lissu hakufanya hivyo jana kutokana na kutakiwa na askari hao aondoke eneo hilo.

Ulinzi uliimarishwa na ni watu wachache waliomlaki kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya polisi kuwazuia wengi katika lango la kuingilia.

Lissu alikamatwa siku tisa zilizopita akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) alikoenda kwa ajili ya safari ya Kigali nchini Rwanda kushiriki mkutano wa wanasheria Afrika Mashariki.

Alisomewa mashtaka siku tatu baadaye akituhumiwa kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais.

Mara baada ya kukamatwa, mmoja wa mawakili wake, Fatma Karume aliiambia Mwananchi kuwa polisi hawakutaka Lissu adhaminiwe kwa madai kuwa upelelezi ulikuwa haujakamilika.

Kabla ya kupelekwa mahakamani, polisi walimpeleka nyumbani kwake na kupekua na baadaye kutaka kuchukua kipimo cha mkojo, jambo ambalo Lissu alikataa kwa hoja kwamba kipimo hicho hakina uhusiano na makosa wanayomtuhumu.

Julai 24, alipelekwa mahakamani lakini hakupewa dhamana baada ya upande wa mashtaka kudai amekuwa akirudia kufanya kosa hilo, huku mawakili wake wakisema hadi sasa hajapatikana na kosa na kwamba polisi wamekuwa wakimkamata tangu mwaka 2015 na hakuna upelelezi uliokamilika hadi sasa.

Lakini jana, Hakimu Mashauri alimpa Lissu dhamana akieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutaja kesi ambayo mwanasheria huyo mkuu wa Chadema amewahi kuruka dhamana.

Hakimu Mashauri alisema hakuna uthibitisho kuwa Lissu aliwahi kuruka dhamana na hiyo haitoshelezi kumuweka mahabusu kwa sababu ya usalama wake.

Hoja ya pili iliyomuweka Lissu nje kwa dhamana ni ile ambayo Hakimu Mashauri aliitaja kuwa ni “upendo wa dhati”.

Alisema Lissu anawakilishwa na mawakili 18, kitu kinachoonyesha wana upendo kwake na ndiyo maana walisimama kidete.

Lissu aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja alisaini dhamana ya Sh10 milioni.

Pia, ametakiwa asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama na wakili wa Serikali, Simon Wankyo alisema upelelezi umekamilika na ameiomba mahakama ipange tarehe kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali na Hakimu Mashauri amepanga asomewe Agosti 24.

Awali, baada ya mahakama kuweka masharti ya dhamana, kesi iliahirishwa kwa muda kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 3:30 kusubiri wadhamini ambao walikuwa wamezuiwa kuingia eneo la mahakama kutokana na ulinzi mkali uliokuwepo jana.

Baadaye, wadhamini waliingia kuwasilisha nyaraka zao, kabla ya Lissu kuachiwa huru na saa 3:50 asubuhi na kuondoka.

Jopo la mawakili wa Serikali linaundwa na Kishenyi Mutalemwa, Wankyo, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo, wakati Lissu anawakilishwa na mawakili 18 wakiongozwa na Karume na Peter Kibatala.

Katika kesi hiyo, Lissu anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Julai 17 akiwa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, aliposema “Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ina ubaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini”.

Chato nao wadhaminiwa

Wakati hayo yakifanyika Dar, Mahakama ya Wilaya ya Chato nayo imetupilia mbali pingamizi la dhamana dhidi ya washtakiwa 51 ambao ni viongozi na wanachama wa Chadema ambao wameshtakiwa kwa kukusanyika katika Kata ya Muganza bila ya kibali. Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Jovith Kato alitoa uamuzi huo juzi baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni marufuku mshtakiwa wa makosa ya jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika.

Washtakiwa hao walidhaminiwa na watu wawili kila mmoja ambao walitakiwa kuweka dhamana ya Sh500,000.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad