Shabiki wa klabu ya Sunderland wa umri wa miaka sita Bradley Lowery, ambaye tatizo lake la kiafya liligusa nyoyo za wengi amefariki dunia.
Bardlay alikuwa anaugua ugonjwa ambao wa Kiingereza hufahamika kama neuroblastoma – aina nadra ya saratani – tangu alipokuwa na umri wa miezi 18.
Bradley alifanywa kuwa kibonzo-nembo wa klabu hiyo na akaunda urafiki wa karibu na mshambuliaji wa klabu hiyo Jermain Defoe.
Aidha, aliongoza wachezaji wa England kuingia uwanjani Wembley wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Lithuania.
Kifo chake kimethibitishwa na wazazi wake kwenye mitandao ya kijamii.
“Kijana wetu mkakamavu ameenda kuwa na malaika leo.
“Alikuwa shujaa wetu na alipigana sana lakini alihitajika kwingine. Hatuna maneno ya kueleza jinsi tulivyohuzunishwa na kifo chake.”
Bradley alipewa matibabu lakini saratani yake ikaibuka tena mwaka jana.
Wahisani walichangisha zaidi ya £700,000 kulipia matibabu yake New York mwaka 2016, lakini madaktari waligundua kwamba saratani yake ilikuwa imeenea sana na hangeweza kutibiwa.
Wazazi wake Gemma na Carl, kutoka Blackhall Colliery, Durham, waliambia Desemba kwamba alikuwa amesalia na “miezi kadha tu ya kuishi”.
Miezi minne baadaye, walifahamishwa kwamba jaribio la mwisho kabisa la kumtibu lilikuwa limefeli.