Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa shtaka la kumshambulia mbunge mwenzake, Juliana Shonza.
Kubenea anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu 240 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 3 katika viwanja vya Bunge mjini hapa.
Kubenea anayewakilishwa na mawakili watano, Jeremia Mtobesya, James ole Millya, Fred Kalonga, Izack Mwaipopo na Dickson Matata, alikana kosa hilo.
Hakimu Karayemaha amesema dhamana kwa mshtakiwa ipo wazi na kumtaka kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na barua kutoka serikali ya mtaa ambaye atasaini bondi ya Sh1 milioni.
Kubenea alikamilisha masharti na kuachiwa kwa dhamana. Pia, ametakiwa kuhudhuria mahakamani bila kukosa isipokuwa kutokana na ugonjwa, kuuguliwa au msiba.
Kutokana na upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi haujakamilika, hakimu ameipanga kesi hiyo kutajwa Julai 26.