Haikuwa ajali, pesa ya ESCROW kupita katika bank ya kanisa katoliki, mgawo kuwafikia mapadre na maaskofu,mawaziri na vigogo wa kila namna katika nchi hii. Ili siku inapobumburuka, basi msururu wa watu ujumuishwe na kuwe na "aibu" ya kuwakamata wote waliohusika.
Harbinder Singh aliitumia njia hii pia,alijenga vituo vya polisi,alikarabati nyumba za viongozi na kuwajengea "mabangaroo" wale aliohisi watamsaidia kuukwepa mkono wa dola.Alinunua pikipiki za doria za polisi,alichangia vifaa na pesa katika mahitaji ya ziada ya jeshi letu la polisi (ushahidi wa picha upo)
Pale Airport ya Dar es Salaam,kuanzia kaunta za VIP mpaka kwenye mlango wa ndege wakati wa kuondoka,wahudumu wote na wafanyakazi walijua leo Singasinga anarudi au anaondoka.Kila alipofika Singasinga au kuondoka,aliachia "tips" bila hiyana. Kuanzia kwa askari wa uhamiaji,check in counter,polisi wa Airport,mbeba mabegi,dereva wa gari la VIP mpaka mfagizi,aliinusa pesa ya singasinga.
Hii ndio maana, Singasinga kabla ya kukamatwa, alishapenyezewa taarifa kuwa anatafutwa kwa muda mrefu ili aweze kukamatwa sababu faili la ESCROW lipo juu ya meza ya "mkuu" na ameagiza kesi ianze ila tu ni lazima hawa wahusika wawili akiwemo singasinga wakamatwe.
Siku ya Ijumaa tarehe 16/06/2017,Seth alikuwa aondoke na ndege ya shirika la ndege la South Africa,flight number SA187 inayotoka Dsm kuelekea Orival Reginald Tambo International Airport,iliyotarajiwa kuondoka saa 1535(masaa ya Afrika Mashariki).Afrika Kusini ndiyo yalipo makazi ya Seth baada ya kupata mgogoro wa kifisadi na kupata shida ya kuishi Nairobi Kenya,alihamia huko Afrika Kusini.
Siku kadhaa kabla ya safari yake ya "ghafla" ya kwenda South Africa,watu kadhaa wa "mfumo" waliokuwa wanapitiwa na mgawo wa Seth, walimtonya mpango wake wa kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Kama kawaida yake, Seth alipitisha mgawo kuhakikisha suala hilo halitokei, kuanzia yule wa chini mpaka wa juu, kila pesa ilipokuwa inamfikia, aliikimbia kwa hoja kuwa "siku hizi sio kama zamani", wote tutakwenda na maji.
Mpaka Ijumaa asubuhi,Harbinder na wapambe wake wakawa wamegonga mwamba katika kila kona walizopita ili kuzuia kupelekwa mahakamani,suluhisho alilopewa na watu wa "mfumo" ambao walikuwa "watii" kwake sababu ya mgawo,ni kuondoka haraka nchini na kukimbilia Afrika Kusini mpaka pale mambo yatakapotulia kama zamani.
Majira ya saa nane mchana,Seth na mwanamke mmoja,walifika eneo la VIP Terminal II tayari kwa safari ya kwenda nje ya nchi ili kukwepa mkono wa mfumo. Eneo la VIP Terminal II hutumiwa na wageni mashuhuri wanaotoka au kuingia ndani ya nchi, Marais, Wabunge,Wawaziri na viongozi wengine wa hadhi ya juu na wafanyabiashara wakubwa hupitia lango hili kwa safari zao.
Seth alikamilisha taratibu zote za safari,kama kawaida yake "tips" za "kimyakimya" zilianzia mlangoni anapoingia na VIP lounge. Kilichomstua kwa haraka ni baadhi ya "tips" zake kukataliwa na baadhi ya wahudumu,alipotoa wengine waliishia kusema tu "Asante".
Taarifa zilishafika mahali husika,kuwa Singasinga yupo Airport tayari kwa safari,akiwa na "boarding pass" mkononi na muda wowote ataingia kwenye ndege tayari kwa safari.
Bila kutarajia,wakati amevuka vihunzi vyote,akiwa anajongea kuingia katika gari la VIP,linalotumika kuwatoa wageni wa VIP eneo la VIP Lounge kuelekea kwenye ndege,ghafla ikatokea gari nyingine,kutoka mahali kusipoeleweka,likiwa limepitia mlango wa dharula na kusimama mkabala na lango la kutokea VIP lounge.
Palepale Harbinder akaamuliwa kuingia kwenye gari hilo lililokuwa na vioo vya giza,na kuachana na benzi la VIP VAN lenye maandishi ya kampuni ya Swissport kwa pembeni,mara moja gari ikageuzwa na kupelekwa kusikojulikana,mpaka mapema Jumatatu,Seth na Rugemalila walipoibukia mahakama ya Kisutu tayari kwa kusomewa mashitaka ya Escrow.
Mchezo wa kumkamata Harbinder hakuwa mdogo,hii ni kwa sababu kwa muda mrefu Harbinder amekuwa anawatumia viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kukwepa mikono ya dola pale anapotakiwa ama kuhojiwa au sakata lake kuibuliwa bungeni.
Safari yake ya kukamatiwa Airport akiwa tayari kuingia kwenye gari kuelekea kwenye ndege,ni matokeo ya kuvujishiwa siri kuwa anatafutwa na anatakiwa kukamatwa,hivyo uwezo wa kuizima kesi haupo zaidi ya yeye kutoroka.
Hii inatupa picha,jinsi ilivyo ngumu kwa kazi hii ya kupambana na "mapapa" aina ya Singh.Inatukumbusha kauli ya Waziri Mkuu Pinda aliposema kuwa,hawa "mafisadi" wana nguvu sana,ukiwakamata nchi lazima itikisike.
Na hakika,kukamatwa kwao,nchi imetikisika,kuanzia Kanisa Kuu la Bukoba alipo Askofu Kilaini mpaka St.Joseph Cathedral Dsm alipo Askofu Nzigilwa.Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Makongo Juu anaposali James Rugemalila mpaka makao makuu ya bank ya Mkombozi hali si shwari.
Viunga vya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nako ni tumbo joto,kuanzia kwa mwenyekiti wa Bunge na baadhi ya wabunge hali si shwari,ofisi za RITA na Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali ni matumbo joto.
Isingelikuwa mkwara wa Magufuli,Harbinder Singh angetutoroka mchana kweupe,na watu wangejiuliza,inakuwaje mahakamani tunamuona James Rugemalila peke yake?Kuna mambo JPM yanamshinda,ila kuna mengine anaamua kiasi unasahau hata yale aliyoharibu.Kumkamata Seth haikuwa kazi ndogo,alinyakuliwa wakati abiria wengine wameshaingia ndani ya ndege,akisubiriwa yeye tu wa VIP.
Hili la Escrow tukipita salama na kushinda,tumshukuru Mungu na tumpe pongezi Rais bila itikadi.Anakumbana na nguvu kubwa sana inayomsaliti katikati ya mapambano,kuna wachache wanauza "ramani ya vita" kwa adui.
By Barafu/Jamii Forums