Katika taarifa hiyo, inaelezwa kuwa Mpinga ameng’olewa baada ya kubadilishwa kituo chake cha kazi, akipangiwa katika eneo lingine, ikiwa ni mwendelezo wa mabadiliko ndani ya jeshi la polisi.
Habari za ndani ambazo Nipashe ilizipata kutoka kwa chanzo chake cha uhakika zilidai kuwa Kamanda Mpinga amebadilishwa kituo chake cha kazi kwa kupelekwa Mbeya kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Kamanda wa Mkoa wa Mbeya,Dhahiri Kidavashari, amerudishwa makao makuu ya jeshi.
Hata hivyo, hadi kufikia jana jioni, Nipashe haikufanikiwa kupata taarifa rasmi za jeshi hilo kuelezea mabadiliko hayo.
Awali, alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa, alisema hawezi kusema taarifa hizo ni za kweli au uongo kwa kuwa hazijamfikia, na kwamba akijulishwa atazitoa bila shida.
Mbali na majibu hayo, Mwakalukwa alimtaka mwandishi amuulize Mpinga mwenyewe ambaye pia ni msemaji.
“Sasa nikuambie kitu, taarifa kama hizo unamuuliza anayehama, yaani Mpinga… maana na yeye ni msemaji.
Halafu kama anahamishwa, yupo ambaye atachukua nafasi yake atakuambia. Mimi ninasemea Jeshi zima hivyo kama amehama na namba zake mnazo, muulizeni,” alisema Mwakalukwa.
Aidha, Mwakalukwa aliongeza: “ Lakini huenda akawa bado … mmesikia fununu tuu. Msifanye kama wale wa social media. Kama umepata hizo fununu, si usubiri mamlaka iseme na uzuri wake tumeruhusu wasemaji ni makamanda wa mikoa na makamanda wa vikosi. Hivyo anaweza kukujibu vizuri,”
Mwandishi alipumuuliza Kamanda Mpinga juu ya kuwapo kwa taarifa za yeye kuhamishiwa Mbeya, alisema: “Mimi natokea safari Dodoma kikazi. Kwa hiyo nitatoa taarifa rasmi leo. Na mimi nimesikia kuna uhamisho ila sijajua nimepangiwa wapi.”
Source: Nipashe