KAMANDA Sirro: Wametaka Ubaya Wataupata

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, amesema watu wanaotumwa kutekeleza mauaji Wilaya  za Kibiti, Mkuranga na Rujifi watajibiwa kwa ubaya na kwamba kuanzia sasa wametangaza vita dhidi yao.

Alisema watu hao ambao wanaua raia na askari walidhani watawachonganisha wananchi kirahisi bila kujua Watanzania wana umoja usioweza kugawanyika.

Sambamba na hilo, amesisitiza kuwa suala la ulinzi ni la watu wote na kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kujilinda kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

IGP Sirro aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akipokea msaada wa magari manne kila moja likiwa na thamani ya Sh. milioni 126.2 kutoka  kampuni ya Haval Great Wall Motors, yatakayosaidia kupatamba na uhalifu nchini.

“Sisi Tanzania hatujazoea vurugu za namna ile kwa hiyo wale ambao walikuwa wametumwa walifikiria Tanzania kama nchi nyingine wataona majibu yake,” alisema.

“Tangu zamani sisi ni wamoja na tunapendana kwa hiyo wale waliokuwa wametumwa vibaya vibaya na sisi tutawajibu kwa ubaya ubaya tu.”

Alisema Jeshi la Polisi linakwenda vizuri na suala la mauaji ya Kibiti na kwamba muda si mrefu kutakuwa na majibu mazuri.

IGP Sirro ambaye aliapishwa na Rais John Magufuli Mei 29, mwaka huu, akichukua nafasi ya Ernest Mangu aliyeondolewa, alisema wenyeviti wa vijiji wa Mkoa wa Pwani wana wajibu wa kuimarisha hali ya ulinzi katika maeneo yao.

“Maeneo hayapitiki, Kibiti, Ikwiriri, Mkuranga hata maeneo mengine ya nchi wananchi wanapaswa kujilinda kwa kuanzisha ulinzi shirikishi,” alisema IGP Sirro.

Alisema matukio ya uhalifu kwa miaka ya sasa yamekuwa magumu kuliko ya miaka ya nyuma, hivyo jeshi hilo linapaswa kwenda na wakati.

Kwa mujibu wa Sirro, Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto  mbalimbali kama vile uhaba wa vitendea kazi, ufinyu wa bajeti na uwapo wa miundombinu mibovu ambayo ni kikwazo kwa polisi kufika sehemu ya tukio kwa haraka.

Naye Meneja wa kampuni iliyotoa magari hayo, Jianguo Liu, alisema wametoa msaada wa magari hayo kwa Jeshi la Polisi kwa lengo la kusaidia kupambana na uhalifu.

Mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani yalianza Januari, 2015 idadi ikitajwa kufikia 39 huku wanaotekeleza mauaji hao wakiwa hawafahamiki.

Mauaji ya mwisho kutekelezwa yalitokea Juni 27, mwaka huu, wilayani Kibiti baada ya watu wawili kuuawa kwa kupigwa risasi katika kijiji cha Mangwi, kata ya Mchukwu wilayani Kibiti usiku, huku mtu mmoja akijeruhiwa vibaya sehemu ya jicho.

Mauaji hayo yalitekelezwa ikiwa imepita wiki moja baada ya askari wawili wa usalama barabarani wilayani Kibiti mkoani Pwani kuuawa kwa kupigwa risasi katika kijiji cha Masafiri kata ya Bungu, huku askari mmoja akisalimika.

Moja ya matukio yaliyowahi kutokea wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani na kuacha historia kwa Jeshi la Polisi ni lile lililotokea Aprili 13, mwaka huu, baada ya askari wanane kushambuliwa wakitoka kubadilishana lindo.

Katika shambulio hilo, majambazi hao walipora bunduki saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.

Kutokana na mwendelezo wa mauaji katika Wilaya hizo, IGP Sirro alipoingia madarakani alitangaza donge nono la Sh. milioni 10 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa 12 wa mauaji.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Abdurshakur Ngande Makeo, Faraj Ismail Nangalava, Anaf Rashid Kapera, Said Ngunde, Omary  Abdallah  Matimbwa, Shaban Kinyangulia,  Haji Ulatule, Hassan Uponda, Rashid Salim Mtulula, Hassan Nasri Mzuzuri na Hassan Njame.

IGP Sirro alitangaza bingo hiyo zikiwa zimepita siku chache tangu Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Onesmo Lyanga alipotangaza bingo ya Sh. milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watu hao.

POLISI KUWEZESHWA
Wakati huo huo, Serikali imesema imeongeza doria na vitendea kazi kwa Askari wa Mkoa Maalum wa Kipolisi wa Rufiji unaoundwa na wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.

Katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema pia tayari Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo maalum ameshateuliwa na kutoa rai kwa wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuwezesha watuhumiwa wote kukamatwa.

Majaliwa alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila raia wa Tanzania, wakiwamo wananchi wa wilaya hizo, wanakuwa huru kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili kurejesha hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na vitendea kazi kwa askari,” alisema Majaliwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad