SERIKALI imetoa onyo kwa watumishi wa umma wanaotoa siri za serikali na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki (pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa watumishi wa umma wa Manispaa ya Ubungo.
Kairuki alisema mtumishi wa umma atayejihusisha na usambazaji wa taarifa za serikali, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani na kupewa kifungo cha miaka 20 jela. Alisema serikali ina utaratibu wake wa kutoa taarifa kwa umma ikiwa ni pamoja na kupitia machapisho yake kwa jamii.