Mbunge wa Ubungo Mh Saed Kubenea wiki iliyopita alifanya mkutano na vyombo vya habari kama Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wa CUF iliyochini ya uongozi wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif na kutangaza oparesheni ya kumuondoa Profesa Lipumba katika ofisi za chama cha CUF Buguruni.
Baada ya Kubenea kutangaza oparesheni hiyo siku mbili mbele aliibuka Profesa Lipumba na kwenda kituo cha polisi kutoa malalamiko juu ya kile alichokisikia kutoka kwa kiongozi huyo na oparesheni hiyo aliyotangaza.
"Ni kweli Kubenea ameitwa na kuitwa kwake kumekuja baada ya wiki iliyopita kufanya mkutano na waandishi wa habari kama Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani akiwa pamoja na viongozi wa CUF inayoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro na Katibu Mkuu Maalim Seif na kutangaza operesheni inayoitwa 'Operesheni Ondoa Msaliti Buguruni (OMB). Operesheni hiyo itaendeshwa kwa ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA" ilisema taarifa ya CHADEMAProfesa Lipumba na baadhi ya viongozi wa CUF wapo katika mgogoro kutokana na kiongozi huyo kipindi cha uchaguzi mwaka 2015 kuandika barua ya kujiuzulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa CUF taifa na kubaki mwanachama wa kawaida, lakini baada ya uchaguzi kupita kiongozi huyo akataka kubatilisha maamuzi yake ya kujiuzulu jambo ambalo viongozi wa CUF na baadhi ya wanachama wamekuwa wakilipinga na kukataa, japo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi yeye bado anamtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF taifa.