Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea amemshukia Spika wa Bunge, Job Ndugai, akimtuhumu kuendelea na tabia ya kuwaonea Wabunge wa vyama vya upinzani hasa chama hicho.
Kubenea amesema Ndugai hatoshi kuendelea kuwa kwenye nafasi hiyo kwa sababu amewahi kupata kashfa ya kumpiga ndugu yake ambaye alikuwa mgombea mwenzake wa nafasi ya ubunge Jimbo la Kongwa. Kubenea alitoa shutuma hizo jana wakati akizungumza na wapiga kura wake katika mkutano wa hadhara kwenye Kata ya Manzese, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisema Ndugai alifanya tukio hilo wakati wa kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015. “Simshangia Ndugai kwa sababu alimchapa ndugu yake, Mgogo mwenzake leo amewafungia wabunge wa upinzani akiwamo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee,” alisema Kubenea.
Mbali na hilo, aliwataka vijana na wanawake kuanzisha vikundi vya VICOBA ili kunufaika na mikopo inayotolewa na Serikali na mfuko wa jimbo hilo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao na kukuza uchumi. Alisema wananchi wa kata hiyo na wa Jimbo la Ubungo wana fursa ya kunufaika na fedha za mfuko wa jimbo ambazo amekuwa akizitoa katika vikundi mbalimbali ili kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Pia aliahidi kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha Polisi cha Manzese ili wananchi wapate ulinzi kutoka kwa Jeshi la Polisi. Diwani wa Kata ya Manzese, Ramadhani Kwangaya, alisema kata hiyo ina vikundi visivyopungua 15 vyenye watu zaidi ya 75 na kila mmoja alipatiwa Sh. 315,000 na zaidi ya Sh. milioni 200 zilitolewa kupitia mfuko wa jimbo.
Alisema shughuli nyingi za miradi ya maendeleo zilichelewa kwa sababu kulikuwa na mgawanyo wa Halmashauri ya Kinondoni na kuwa na Halmashauri mbili ya Ubungo na Kinondoni. “Msishangae kimya kirefu bila kuwa na mradi. Manispaa mpya ya Ubungo ilianza Novemba mwaka jana na shughuli rasmi zilianza Januari mwaka huu. Hivyo tulichelewa kurejea kwenu kuwaeleza kile tulichokusanya na kuanza kutekeleza na ndio sababu ilifanya miradi mingi katika kata yetu kuchelewa,” alisema Kwangaya.