Lile sakata la mwanamama Asma Juma (29) aliyedai kujifungua watoto wawili mapacha katika Hospitali ya Temeke Machi mwaka huu, limechukua sura mpya baada ya familia yao kusema italifikisha suala hilo kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli ili kupatiwa suluhisho.
Hatua ya familia hiyo inatokana na kutoridhishwa na ripoti iliyotolewa na timu iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambayo ilidai baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika kuwa mama huyo alijifungua mtoto mmoja, tofauti na madai yake kuwa alikuwa na ujauzito wa mapacha wawili.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko jana, mama huyo alisema yeye na mumewe, hawajakubaliana hata kidogo na ripoti hiyo iliyotolewa siku chache zilizopita na kwamba msimamo wao upo palepale.
“Ile ripoti iliniumiza mno, ni ngumu kwangu kukubaliana nayo, tumeona bora kwenda kwenye haki za binadamu ili watusaidie swala letu, kwa mujibu wa ripoti hiyo inasema sikuzaa mapacha ila kosa la hospitali lipo kwenye kipimo, si sawa,” alisema.
Naye mumewe, Abubakar Pazi alisema kamwe hawezi kukubaliana na majibu hayo, ndiyo maana ameona uamuzi mzuri ni kwenda haki za binadamu ili wasaidiwe na kama haitoshi, atafika hadi ikulu akamuone Rais Magufuli.
“Kitu kilichoniumiza kwenye hiyo ripoti ni kusema mke wangu hakuzaa watoto wawili, kwamba hospitali watawajibika kwa kukosea kipimo tu, naona si sawa, niliomba ile ripoti baada ya kusomwa nipewe ili na sisi tuwe nayo, lakini tumenyimwa, tunatafuta njia ya kumfikia rais hata kwa kumuandikia barua atusaidie hili suala,” alisema.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke hakupatikana ili kuzungumzia suala hilo, lakini Msaidizi wake, Dk. Emmanuel Salakisha ambaye ndiye msemaji wake, alisema kwa sasa hawana la kusema kwa vile lilishavuka ngazi yao.
“Kilichoonekana kwenye ile ripoti, kipimo kilikosewa kwenye ile hospitali waliyopima mwanzo, kuhusu hayo mambo ya kwenda haki za binadamu bado hatujapata taarifa, hata hivyo hilo jambo lilishavuka kwenye ngazi yetu, lipo ngazi ya wizara, kama likija huku kwetu tutawapa ushirikiano,” alisema.
Sakata la mama huyo lilianza Machi mwaka huu baada ya kudai kuwa madaktari katika Hospitali ya Temeke walimuibia mtoto wake mmoja, kwani siku zote za ujauzito wake, aliamini ana watoto mapacha kutokana na vipimo alivyofanyiwa katika hospitali binafsi ya Huruma, iliyopo Mbande.
Baada ya mama huyo kuhoji juu ya tukio hilo, madaktari wa Temeke walimweleza kuwa vipimo alivyofanyiwa awali vilikosewa, kitu ambacho wamekuwa wakikipinga kwa muda wote.
Lile Sakata la Mama Kuibiwa Mtoto Kutua kwa JPM
0
July 26, 2017
Tags