Mkutano huo uliofanyika wiki jana mkoani Dodoma chini ya uongozi wa Askofu Mkuu wa Jimbo, Jacob Erasto Chimeledya, ulifikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa mgogoro wa uongozi wa muda mrefu katika dayosis hiyo iliyoko mkoani Mwanza.
Askofu Mkuu, Chimeledya amesema kwamba baraza hilo limefikis uamuzi huo baada ya kulazimika kupiga kura ili kufikia azimio ambapo maaskofu 25 waliunga mkono na maaskofu 3 kupinga.
"Baada ya matokeo hayo ya kura, baraza limenipatia jukumu la kusimamia utekelezaji wa azimio hilo kwa kuandaa ratiba ya kuachia madaraka kwa amani" alithibitisha Askofu Chimeledya.
Apoulizwa kuhusu azimio hilo la maaskofu wenzake, Askofu Kwangu wa DVN alikiri kuwepo kwa azimio hilo lakini akadai kuwa uamuzi wa kujiuzulu atauchukua endapo ataona unafaa. "Mgogoro wenyewe sio mkubwa kihivyo ila nitaangalia na kuamua, sidhani kama kunasababu ya mimi kujiuzulu" alisema Kwangu na kuongeza kuwa wanaompinga ni wakristo wachache pamoja na baadhi ya wachungaji.
Akithibitisha kuwepo kwa azimio hilo, Askofu wa dayosis ya Ruvuma, R. Haule, amesema kuwa mgogoro huo wa DVN unalichafua kanisa la Tanzania na hivyo wamemtaka Kwangu ajiuzulu.
"Tumepiga kura na maamuzi yanamtaka ajiuzulu kwa amani na heshima ili jina la Mungu litukuzwe" alisema Askofu Haule.
Mgogoro huo ambao umelidhoofisha kanisa la DVN limeshika kasi katika siku za karibuni ambapo waumini wa kanisa hilo walimpiga marufuku Askofu huyo kuabudu kwenye kanisa kuu (cathedral) na makanisa mengine kwenye parishi 40 kati ya 47 na pia kumnyang'anya gari moja aina ya Suzuki Vitara.