Msemo huu unanifanya nimfikirie kwa kina Mfalme wa Bongo Fleva, Alikiba kama mwenyewe anavyojiita King Kiba, kuwa ni kweli hasikii wala kusoma maoni ya mashabiki wake?, mashabiki ambao kila uchao wanaolia atoe wimbo mpya huku yeye akiendelea kupuuzia kilio chao na kuwaacha mashavu yao yakilowa machozi.
Bila shaka yoyote AliKiba kama utaendelea na mwendo wako wa kutoa ngoma moja kila mwaka kwa soko la muziki jinsi lilivyo hapa barani Afrika utasahaulika kwa kizazi hiki ambacho hakishabikii msanii bali kinashabikia kazi unazotoa.
Anyway inawezekana ukawa bado una mtazamo wako wa kutopangiwa na mtu kama ulivyosema siku moja kwenye mahojiano yako na kituo cha Radio cha Kiss FM cha nchini Kenya, nanukuu “sitaki kuwasikiliza hao kwa sababu nina Target yangu ninavitu vya kufuatilia sitaki hata mtu yeyote aniingilie kwenye Target yangu kwahiyo kama utawafuatilia utapotea sifanyi muziki kwa kushindana kama hao watafanya muziki kwa kushindana nitawaacha washindane “
Hapo nilianza kupata mashaka baada ya kusikiliza mahojiano yako kuwa hutaki kuwasikiliza mashabiki wako na hufanyi muziki wa kushindana, Je muziki unaoufanya ni muziki wa aina gani na nini? na kwanini uhangaike kila siku kwenda kushoot video nje ya nchi ile hali muziki wako sio wa ushindani?
Mosi kauli ya kusema unafanya muziki bila ushindani naifananisha na ile inayosema nafanya muziki for fun ambayo mpaka sasa sijaisikia tena kwani hata waimbaji wa muziki wa kisingeli nao wenyewe wanaushindani hii yote ili kuleta ladha ya muziki.
Pili kama utakuwa unafanya muziki usiokuwa na ushindani basi tukubaliane na wewe kuwa muziki wako pia sio biashara unafanya kwa kujifurahisha kitu ambacho kiuhalisia kina kinzana na kauli yako.
Kilio cha mashabiki wako
Ni mwaka sasa umepita AliKiba hajatoa ngoma kitu ambacho kwa muziki wetu wa kiafrika ni rahisi sana kusahaulika kwenye soko kwani mashabiki wengi wa muziki hawaangalii Msanii anafanya biashara gani nje ya muziki bali huangalia ana nyimbo gani katoa na kuanza kumsikiliza hii ni tofauti na mashabiki wa Ulaya au Marekani.
Kitu ambacho Alikiba ameshindwa kuendana nacho ni kukaa muda mrefu bila kutoa nyimbo kitu ambacho mashabiki wake hufikia muda na kuanza kumsahau huku akiwaahidi kuendelea kusubiri na ahadi ya kuku kwa vifaranga wake kuwa “ipo siku nitawapa maziwa”.
Pitia maoni ya baadhi ya mashabiki wake jinsi wanavyoumizwa na ahadi zake za ngoja ngoja kwenye mitandao ya kijamii.
andesyzabron360Yani alikiba tumekuchoka xana yani wewe msanii gani unashindwa na wasanii wachanga hebu angalia hata Asley anakushinda kila Siku anatoa ngoma juu ya ngoma wewe unabakikucheza na TEMBO tumekuchoka xaxa tunahamia WASAFI kupiga selfu na TIFA wewe cheza na tembo TU
___aysher___the___modestyYaani ALIKIBA yupo SLOW sana na mashabiki ndo wanampa kiburi kumsifia ujinga Hivi msanii gani ukae mwaka mzima nyimbo mpya huna kiki huna Ukiulizwa eti mziki ni business biashara gani Hyo huleti bidhaa mpya kwa wateja wako endelea kukaa kimya me saivi TEAM MZIKI MZURI No matter nani ameimba Bora univutie tu!
chugaellynaandika sms hii huku moyo wangu ukisononeka nimepitia sms za mashabiki wezangu nikagundua tulioumia kisa ali kiba kuto achia ngoma ni wengi na nina apaa itakuwa nimwazo namwisho kuku fatilia tena mpaka pale utapotoa sababu yenye kueleweka nn chazo chakuchelewesha ngomaHaya ni baadhi ya maoni ya mashabiki wako ambao mamilioni ya mashabiki wanasononeka, sitaki kuamini kama Alikiba husikii kilio cha mashabiki hawa ambao asilimia kubwa uvumilivu umewashinda kwa ngoja ngoja zako.
Kwanini Davido au Aslay?
Davido mwanzoni mwa mwaka 2016 alivyosainiwa na Sony alikaa karibia mwaka bila kuachia ngoma, kitendo ambacho mashabiki wake walianza kumuandama mitandaoni wakimshinikiza kutemana na Sony kama wanambana asiachie ngoma kitu ambacho hata Davido mwenyewe alianza kuona kinampoteza na alijaribu kuonesha hisia zake kuwa hakufurahia hali ile kwani alianza kupoteza mashabiki.
Baada ya malalamiko hayo Davido akaanza kurejea kwenye maisha yake ya kawaida na kuanza kuachia ngoma juu ngoma ambapo kuanzia Novemba mwaka jana hadi Julai mwaka huu, tayari kaachia nyimbo nne ambazo zimemfanya mwaka huu kupokelewa vizuri zaidi tofauti na mwaka jana ambapo hata yeye mwenyewe alikiri muziki wake uliyumba kutokana na kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutoa ngoma kitu ambacho kilimfanya hadi kukosa nominations kwenye tuzo kubwa duniani.
Kwa hiyo Alikiba ni vema ukatumia kilio cha mashabiki wako kiwe kama chachu ya kudondosha ngoma kali kwa muda kwani ni Wasanii wachache sana wanaolazimishwa na mashabiki wao kuachia ngoma na ni bahati kwako kwani wapo wasanii wengi hawatoi ngoma na bado hawaulizwi na mashabiki wao.
Kama kwa Davido ni mbali basi jifunze kwa Aslay ambaye baada ya kundi la Yamoto Band kuyumba kwa mwaka mmoja huku watu wengi wakiamini kuwa kundi hilo limekufa pamoja na wasanii wake ambao walikuwa wakitoa ngoma kila mwezi kipindi cha nyuma. Nakumbuka wakati anatangaza kuwa ataanza kuachia ngoma zake kama Solo Artist wengi walimbeza kuwa hawezi kurudi kama miaka ya nyuma alivyokuwa akifanya muziki peke yake kabla ya Yamoto Band.
“Nawahakikishia mashabiki wangu nitarudi kama zamani kwani hapa katikati tulisimama kidogo ila kwa sasa nitatoa ngoma kama Solo Artist”,alisema Aslay kwenye mahojiano yake na kituo cha redio cha Clouds Fm.
Baada ya hapo Aslay akaanza kuwarudisha mashabiki wake kwa kuachia ngoma juu ya ngoma yaani kuanzia Januari mpaka Julai mwaka huu tayari ameachia ngoma kubwa tano kitu ambacho kwa sasa ukipita kila mitaani, ukisikiliza Radio au kutazama TV hauwezi kukwepa kukutana na ngoma zake hicho ndio kitu mashabiki wanataka, na sio ahadi nyingi.
Ushauri wangu kwa Alikiba
Mosi, Alikiba jifunze kuchukua na kuyafanyia kazi maoni ya mashabiki wako kwani hao ndiyo wamekufanya ufike hapo ulipo usipuuze kwani mtaji wa msanii yeyote duniani ni mashabiki wake.
Pili, kwa aina ya mashabiki wa muziki wa Afrika hususani Tanzania hawaangalii unafanya nini nje ya muziki wako, wanachoangalia ni ngoma tu ndio maana hata Davido alivyokuwa kimya mashabiki walimuandama mitandaoni wakidai atoe ngoma haimaanishi alikuwa hafanyi show au hakuwa na biashara nyingine ila mashabiki wake walitaka kusikia ngoma kutoka kwake.
Tatu, sitaki kuamini kuwa una Menejimenti mbovu kiasi hicho, mimi ninachoamini ni kwamba una Menejimenti nzuri ambayo inauwezo wa kila kitu hivyo ni bora ukawapa taarifa kama Davido alivyowachana ili wakupe muda wa kutoa ngoma kwa wakati, Alikiba wewe sio Msanii wa kukaa mwaka mmoja na wimbo mmoja wa AJE bila kutoa ngoma nyingine mpya ni maumivu kwa sisi mashabiki wako ambao tunataka kazi tuu na sio ahadi.
Naamini baada ya makala haya Alikiba na Menejimenti yako mtawapoza maumivu mashabiki wenu kwa kuachia ngoma mpya kwani wanaumia na nyie hamsikilizi vilio vyao mnaacha machozi yao yanafutwa na wasanii wengine ambao ni washindani wenu wakubwa.