RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amejiuzulu wadhifa wake wa Ujumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kupitia kwa wakili wake, kampuni ya Rwegoshora, Malinzi amewaandikia barua FIFA kuwataarifu kujitoa kwenye Kamati hiyo kutokana na kuwa mikononi mwa dola kwa sasa.
Malinzi, pamoja na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga.
wapo rumande hadi Julai 17, upepelezi wa kesi yao utakapokamilika baada ya kunyimwa dhamana Julai 3 katika kesi inayowakabili.
Watatu hao walipandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Juni 29 na kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Katika kesi hiyo, Serikali inawakilishwa na jopo la mawakili watano, wakiongozwa na Pius Hila huku upande wa washtakiwa ukiwakilishwa na mawakili watano, wakiongozwa na Jerome Msemwa.
Mawakili hao watano kwa pamoja wameshindwa kuafikiana ili washitakiwa wapatiwe dhamana.
Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguurma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
Lakini kwa mwenendo wa kesi, Malinzi ndiyo kama amekwishaaga TFF, kwani uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma naye hatashiriki tena kutokana na kukosekana kwenye usaili.