Mama ntilie Tinga kwa Mbunge na Sufuria zenye Ugali


Mama ntilie mmoja amebeba masufuria ya chakula na kuyapeleka katika mkutano wa hadhara ili kumuonyesha mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly namna alivyopata hasara baada ya watendaji wa halmashauri ya manispaa hiyo, kumzuia asifanye biashara yake.


Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Rhoda Mwalukomo amekuwa akiuza chakula chake katika chumba kilichopo kando ya barabara ya kuingia stendi kuu ya mabasi Soko Matola, ambako mbunge huyo alikuwa akifanya mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu.


Rhoda, ambaye awali alipewa nafasi ya kuelezea kero yake jinsi anavyonyanyaswa na mmoja wa watendaji wa idara ya afya wa manispaa hiyo, aliona maelezo yake hayatoshelezi ndipo alipoamua kwenda kuvunja kufuli ambalo lilifungwa katika chumba hicho na kubeba chakula kilichokuwepo na kukipeleka katika mkutano huo.


Baada ya kufika katika eneo la mkutano huo, mbunge Hilaly na baadhi ya wananchi waliofika walionyesha simanzi jinsi ambavyo wingi wa chakula kilichokuwemo katika masufuria hayo kikianza kuharibika kutokana na kuzuiwa asifanye biashara hiyo tangu majuzi kwa madai anatakiwa kufanya ukarabati kadri kanuni za afya zinavyoelekeza ndipo aendelee na biashara hiyo.


Rhoda akizungumza huku akitokwa na machozi alimweleza mbunge huyo kwamba mara baada ya kuzuiwa kufanya biashara yake hadi afanye ukarabati kadri alivyoelekezwa na afisa afya huyo, alitii na kufanya ukarabati lakini baadaye afisa afya huyo alimhoji kwanini amefanya ukarabati kwa haraka namna hiyo, “sisi tunataka ufunge ndio ufanye ukarabati taratibu,” kitu ambacho Rhoda anadai ni uonevu dhidi yake.


Alimuomba mbunge huyo kuona namna ya kumsaidia ili aweze kuendelea na biashara yake, pamoja na kwamba amepata hasara ya zaidi ya Sh 120,000 kutokana na chakula ambacho atalazimika kukimwaga ambacho ni wali, pilau, nyama ya kuku, ng’ombe, samaki na ugali.


Aidha, Mbunge Hilaly amesema kuwa amewasiliana na ofisa afya huyo na amekiri kufunga biashara ya mama huyo kwa madai anapaswa kutekeleza maagizo ya kanuni za afya ndipo watakapokwenda kukagua na wakijiridhisha kwamba amezingatia kanuni za afya ndipo watafungua biashara hiyo.


Mbunge huyo amesema licha ya kwamba leo (jana) so siku ya kazi lakini wamekubaliana na afisa huyo kufika katika chumba cha biashara ya mama huyo na kuona uwezekano wa kuifungua biashara hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad