MANJI Aondolewa Muhimbili Usiku Apelekwa Keko, Adaiwa Kuchukuliwa Chini ya Ulinzi Mkali

Mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji, ameondolewa chini ya ulinzi mkali wa Polisi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu na kupelekwa Gereza la Keko, lililopo jijini Dar es salaam.

Taarifa za uhakika na ambazo zimethibitishwa na wakili wake, zinaeleza kuwa, Manji, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na Usalama wa Taifa ambayo kimsingi hayana dhamana, aliondolewa hospitalini hapo juzi saa moja jioni.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya gereza la Keko na ndani ya Taasisi ya JKCI, vililithibitishia Mtanzania jumamosi juu ya taarifa hizo za Manji.

"Ni kweli Manji walimwondoa jana usiku, alipelekwa moja kwa moja Gereza la Keko", alisema mmoja wa watoa taarifa.

Katika kuthibitisha hilo Mtanzania Ijumaa jana lilifika JKCI, lakini halikuwaona askari magereza waliokuwapo hapo kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa siku zote ambazo Manji alikuwa amelazwa.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janab, ambaye hata hivyo alikataa kuthibitisha taarifa hizo, kwa madai kuwa, hawezi kutoa taarifa za mgonjwa kwa kuwa si utaratibu.

"Si utaratibu wetu kutoa taarifa za mgonjwa... labda nikuambie tu jambo la msingi na kubwa sisi leo tupo katika viwanja vya Sabasaba, tumewapima watu takribani 420 hivi magonjwa ya moyo na wapo ambao walikuwa hawajui wanaumwa na tumewaambiwa waanze dawa", alisema Profesa Janabi.

Mtanzania lilimtafuta kwa njia ya simu mmoja wa mawakili wa Manji, Alex Mgongolwa, ambaye alisema alikuwa hospitali akimuuguza mama yake, hivyo hakuwa na taarifa hizo.

Wakili Mgongolwa alimtaka mwandishi wa gazeti hili kumtafuta Wakili Hudson Ndusyepo, ambaye ni miongoni mwa wanaomtetea Manji, ili kupata taarifa za kina.

Mtanzania liliwasiliana na Ndusyepo, ambaye alithibitisha taarifa za kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

"Ninaweza kuthibitisha ni kweli amekuwa discharged (ameruhusiwa) kutoka hospitali na ninaweza kuthibitisha kuwa ni kweli tupo Keko, ila suala la kama ametoka jana au juzi kupelekwa Keko silijui, kwa sababu leo ni mapumziko", alisema Wakili Ndusyepo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad