Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Argentina na klabu ya Fiorentina, Gabriel Batistuta ameweka wazi kwamba kwa sasa anapata shida kutembea baada ya kucheza mpira wa miguu kwa miaka 17.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 48 sasa alistaafu soka mwaka 2005 baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa sana, akiifungia klabu yake ya Fiorentina magoli 168 na magoli 56 kwa timu yake ya Taifa.
Lakini amekaririwa na mtandao wa Shirikisho la Mchezo wa Soka Ulimwenguni Fifa.com kwamba “sasa anapata shida kutembea ” kwa sababu ya juhudi kubwa alizokuwa akizielekeza kujiimarisha kisoka ujanani.
“Nilikuwa nafanya kazi kubwa sana zaidi hata ya nilivyotakiwa kufanya,” amekaririwa Batistuta.
Mwaka 2014, Batistuta alisema kuwa aliwaomba madaktari wamkate miguu yake yote kwa sababu ya maumivu makali aliyokuwa akiyapata.
Hali yake ilikuwa imara kwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa kupunguza msuguano katika mifupa na vifundo vya miguu lakini imemuacha akiwa na tabu katika kutembea.