Rais wa UFC, Dana White (katikati) akijaribu kuwatenganisha Floyd Mayweather (kushoto) na Conor McGregor wasipigane 'kavu kavu' usiku wa jana ukumbi wa LA's Staples Center mjini Los Angeles, Marekani
MPIGANAJI Conor McGregor ametamba kummaliza katika raundi ya nne bingwa wa dunia wa ngumi za kulipwa ambaye hajawahi kupoteza pambano, Floyd Mayweather katika ufunguzi wa ziara ya promosheni ya pambano lao la Agost 26, mwaka huu mjini Los Angeles, Marekani.
Mbele ya mashabiki 11,000 ukumbi wa LA's Staples Center, Mayweather na McGregor walikutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza tangu kuthibitishwa kwa pambano lao la utajiri mkubwa.
Licha ya kutokea mbele ya umati wa mashabiki wa nyumbani na kuvaa tracksuti yenye rangi za bendera ya Marekani, lakini Mayweather alijikiuta akizomewa huku mpinzani wake kutoka Ireland, McGregor akishangiliwa kila alipotokea kwenye kioo kikubwa chaTelevisheni.
"Atazimika ndani ya raundi nne. Hana uzoefu wa hii. Simuogopi. Huu ni mchezo wenye sheria zinazokubana na kulifanya hili liwe nusu pambano. Kama hili lingekuwa pambano, asingemaliza raundi hata moja,"alisema McGregor akimaanisha wangepigana katika mchezo wake wa UFC wa kuchanganya na mateke angemmaliza mapema zaidi Mayweather.
Lakini 'bishoo' Mayweather naye hakuwa kimya, kwani alijibu tambo za mpiganaji huyo mwenye umri wa miaka 28 anayejiandaa kwa pambano la kwanza kabisa la ngumi bila mateke kiasi cha wawili hao kukaribia kupigana 'kavu kavu'.
"Ni bwana mdogo, yupo katika miaka ya 20, nipo katika miaka ya 40. Damu yake inacheka, siyo mimi" alisema Mayweather ambaye pia alidai pambano hilo lina mvuto mkubwa wa kishabiki.
"Nimekuwa nikifanya hivi kwa miaka 20. Nimekuwa hapa kabla. Lakini ni mgumu. Ni shujaa. Bora lazima apigane na bora. Mashabiki wamelitaka pambano hili, McGregor amelitaka pambano hili, nimelitaka hili pambano. Agost 26 itakuwa machozi, jasho na damu tangu kengele ya ufunguzi," amesema.