INAWEZEKANA ikawa ni vizuri sana kuwa mtu ambaye unajivunia sana kujua lugha ya wenzako wakati ya kwako huijui vizuri? Mtu gani ambaye angeweza kufurahia kukijua Kingereza wakati akiwa debe tupu unapozungumzia lugha yake ya Kiswahili! Hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga alionekana kushindwa kujibu maswali ya Kingereza aliyoulizwa na mtangazaji wa SuperSport ya Afrika Kusini.
Mara baada ya mechi ya mshindi wa tatu ya michuano ya Cosafa ambayo Tanzania iliing’oa Lesotho kwa mikwaju ya penalti 4-2 na kushika nafasi ya tatu, ndipo alipohojiwa na kuonekana kweli alipishana na maswali. Kwa hali ya kawaida ilionekana Mayanga anaweza kuwa anajua Kingereza cha kubabia kama Watanzania wengi tulivyo.
Lakini kasi ya uzungumzaji ya mtangazaji huyo mwanadada ambaye kawaida anaangalia muda wa runingani, ilimfanya ashindwe kuelewa ameulizwa nini.
Baada ya hapo, baadhi ya Watanzania ambao ninaamini hawakijui Kingereza hata zaidi ya Mayanga walianza kukisambaza kipande cha video ya Mayanga akishindwa kujibu swali hilo na kutaka kuamsha mjadala.
Mjadala ambao mimi hakika nauona ni wa kijinga sana, usio na maana hata kidogo na ambao unatufanya tuonekane ni watu tusiokua kwa kuwa bado tunaamini Kingereza ndiyo kila kitu katika maisha ya mtu aliyefanikiwa. Siku chache kabla, Elius Maguri aliulizwa Kingereza akajibu Kiswahili.
Mjadala tena ukazushwa, wengi wakaanza kuhoji kwa nini ajibu kwa Kiswahili wakati aliulizwa kwa Kingereza. Sisi Watanzania tunataka nini hasa? Aliyejibu kwa Kiswahili tumemuamshia mjadala tukiamini anakosea sana.
Aliyejibu kwa Kingereza cha kubabia, naye anaonekana alikosea sana na wengine wanasema angejibu kwa Kiswahili! Itafikia tupeleke maombi ya kupeleka walimu wa Kingereza katika shule za sekondari kuwa makocha ili waweze kujibu Kingereza baada ya mechi. Nenda Ujerumani, utashangaa wasivyo na habari na hicho Kingereza, nenda Hispania ndiyo utashangaa kabisa. Kweli wao ni wakubwa kimaendeleo.
Sasa Kiswahili kitakua lini kama tutaendelea kuzodoana kama mtu anayezungumza Kiswahili ataonekana hafai? Ukiwa Afrika Kusini, mara nyingi wenyeji wanakusisitiza kuzungumza Kizulu au Xhosa. Lugha mbili kubwa zaidi nchini humo hasa kama watakuona ni mweusi.
Wanataka Kingereza waachiwe Wazungu na wale wanaowaita ‘Makaladi’. Sasa shida iko wapi kujiamini katika lugha yetu? Tunachekana sana hadi inafikia Kiswahili kinaonekana ni kama ushamba kukizungumza runingani hasa inapokuwa katika michuano ya kimataifa! Huenda Mayanga naye alishindwa kujiamini kwa hofu ya kuonekana alizungumza Kingereza. Lakini alipaswa kuachana na hofu ya Kingereza chao, sahihi kabisa na mwisho kama akipata nafasi kama hiyo asiwe na hofu, atandike Kiswahili cha kutosha. Wengi waliomzodoa na kumbeza eti hakuongeza Kiswahili, hawakutumia njia nzuri zaidi ya kutaka kuonyesha kakosea sana huku wengi nawajua Kingereza pia kinawapiga chenga na hawawezi kuzungumza kwa majibizano ya zaidi ya dakika tano maana lazima “umeme utakata”. Waandaaji wa michuano yoyo
te kama Cosafa nao wanatakiwa kuweka nafasi kwa mahojiano ya Kiswahili. Safari nyingine kama Stars itaalikwa, basi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inapaswa kuonyesha inakithamini Kiswahili na kuhakikisha kunakuwa na wakalimani.
Mimi sitamzodoa yeyote aliyezungumza Kingereza cha kubabia, badala yake nitampongeza na kumsisitiza kuzungumza Kiswahili safi mbele ya wanaoweza kukisikia na siku moja wajifunze. Tuachane na zile hisia kwamba anayezungumza Kiswahili hawezi kuwa msomi, mjanja au mtu anayejitambua. Siku hizi mambo yamebadilika, kujivunia Kingereza kupita kiasi nao ni ushamba tu. Kwa wanaopata bahati ya kusafiri wataungana nami. Vizuri kujifunza Kingereza na lugha nyingine, lakini Kiswahili kiwe nembo ya Mtanzania. Badilikeni.
Stori: Saleh Ally Simu: +255 654 948888 Email: salehkubwa@gmail.com