Mpasuko Kanisa la Anglicana Waendelea....Mwanza Kimenuka

KANISA la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza jijini Mwanza, limeingia katika mgogoro mkubwa baada ya Wazee wa Nyumba ya Walei kumwandikia barua Askofu Mkuu, Dk. Jacob Chimeledya na baraza lake la maaskofu wakitaka wamuondoe madarakani Askofu Boniface Kwangu wa dayosisi hiyo.
Katika maelezo yao, waumini hao walisema kuwa, wamechukua uamuzi huo ili kumaliza mgogoro uliodumu katika kanisa hilo kwa zaidi ya miaka miwili sasa wakimtuhumu kiongozi huyo kutumia madaraka vibaya na kufuja mali za kanisa.

Baada ya ibada ya wiki iliyopita katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Nicholaus jijini hapa, Mwenyekiti wa Baraza la Walei Dayosisi ya Victoria Nyanza, Osoro Nyawanga alisema kuwa, barua hiyo inamuomba Askofu Dk. Chimeledya katika kikao cha baraza lake mgogoro huo uwe moja ya ajenda katika mkutano mkuu wa baraza la maaskofu uliotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma.



“Nyumba ya walei tulishamkataa Askofu Kwangu baada ya kushindwa kuliongoza kanisa. Tunaiomba mamlaka kuchukua hatua haraka zaidi kulinusuru kanisa na mali zake,” alisema Nyawanga.

Askofu Kwangu alipopigiwa simu baada ya mwandishi kujitambulisha alijibu kifupi: “Nipo kwenye shughuli nyingine zaidi, naomba unitafute siku nyingine.”

Askofu Dk. Chimeledya alipoulizwa kuhusu barua hiyo alisema hajaiona, lakini akafafanua kuwa kama ipo, kuna utaratibu wa kupitia makao makuu ya ofisi iliyopo Dodoma.

Alipoulizwa kama suala hilo litakuwa kwenye ajenda alisema: “Kama tukiona jambo hilo liwe ajenda, sawa, itategemea na zitakazokuwepo ila hawawezi wao kututengenezea ajenda.”
Mgogoro huo katika kanisa hilo una zaidi ya miaka miwili na tayari uongozi wa kanisa hilo umemfungulia kesi polisi Askofu Kwangu na wenzake wanne, tangu mwaka 2016 na kupewa jalada la kesi namba MW/ RB/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa.

UWAZI
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad