Mtanzania Akimbia Mshahara wa Sh 400 Milioni Marekani...Arudi Tanzania

Kwa uamuzi huu, huwezi kuhoji kiwango cha uzalendo cha Benjamin Fernandes, Mtanzania wa kwanza kuhitimu shahada ya uzamili Chuo Kikuu cha Biashara Stanford nchini Marekani.

Fernandes, ambaye awali alikuwa mtangazaji wa televisheni, ameeleza siri ya kukataa mshahara wa Sh425 milioni kwa mwaka na  badala yake kurudi Tanzania kujenga Taifa.

Baada ya kumaliza masomo yake Marekani, Fernandes alikuwa akifanya kazi katika taasisi ya tajiri namba moja duniani, Bill Gates iitwayo Bill and Melinda Gates Foundation. Sasa ameamua kuacha kazi yenye mshahara mnono na kurejea nchini kusaidia vijana.

Fernandes pia alikuwa akikaa meza moja na mmiliki wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg alipokuwa akifanya kazi katika taasisi hiyo ya familia ya Gates.

Akihojiwa na televisheni ya Millard Ayo, Fernandes alisema kampuni mbalimbali Marekani zinamtafuta kwa ajili ya kwenda kufanya kazi kwa ahadi ya mshahara mnono, lakini amekataa kwa kuwa anataka kuwasaidia Watanzania.

“Watu wengi wananiuliza kwanini nimerudi nyumbani. Ni kweli nilikuwa napewa offer (dau) ya Sh425 milioni kufanya kazi kampuni mbalimbali Marekani, lakini huwa nilikuwa nawaambia nimesharudi nyumbani. Mimi motivation (motisha) yangu si hela ila upendo kwa nchi yangu,” alisema Fernandes.

Alisema alifikia uamuzi huo akijua kuna changamoto atakazokutana nazo.

Alisema ana mpango wa kuwatengenezea njia vijana ili elimu yao iwe msaada kwa jamii.

“Nasikitika watu wananipigia simu wananimbia nina vyeti hivi na hivi, mimi sijali sana elimu yako. Kapige kazi kwa bidii na hiyo kazi itakuheshimu,” alisema Fernandes.

Alieleza asilimia 70 ya watu  ni vijana wenye umri chini ya miaka 25 ambao wanatakiwa kuwa na  mchango katika maendeleo.

Fernandes alisema anataka kuonyesha jinsi teknolojia inavyoweza kuwa msaada kwa kutumia simu za kisasa zinazotumiwa na watu takribani 11.5 milioni nchini.

Aliiomba Serikali kusaidia vijana ili wawe chachu kwa ajili ya mafanikio ya wengine.

“Vijana wanatakiwa watamani kuwa mtu fulani, jambo ambalo linasaidia watoto kukua  na kutimiza ndoto zao,” alisema.

Fernandes alisema endapo atakutana na Rais John Magufuli, atakuwa na mengi ya kumwambia  hasa maendeleo ya Taifa.

“Kwa mfano, nitamshauri Rais kuimarisha mahusiano mazuri na sekta binafsi, biashara na Serikali kuzingatia sheria ili kukuza uchumi na kufanya biashara kuwa nyingi nchini.

Alisema teknolojia bado haijapewa kipaumbele ili kusaidia wanaoishi vijijini na kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa watoto wadogo walio na umri chini ya miaka 10 wanaoweza kuwa chachu ya maendeleo.

“Kitu cha nne ningeshauri Serikali iwasikilize wawekezaji wa nje ili sisi kama nchi tufaidike. Kingine ni nidhamu ambayo Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inazingatiwa hivyo ahakikishe vijana wanakuwa na nidhami,” alisema Fernandes.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Hamis Mwinyimvua alisema ni jambo zuri kwa Watanzania wanaosoma nje ya nchi kurudi na kuleta ujuzi wao nchini.

“Kama amejisomesha kwa fedha zake, anaweza kurudi au kuamua kubaki, lakini kikubwa anaweza kufanya kama wafanyavyo diaspora (wazawa wanaoishi nje), fedha wanazopata zinatumwa Tanzania na zinatumika kwa maendeleo,” alisema.

 Mwananchi
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Nilishawahi pia kusoma habari za huyu kijana katika mitandao ya kijamii mingine ya kitanzania na kushangazwa na maoni ya hovyo ya kumbeza kutoka kwa watanzania na la kushangaza ni kutokana kuwa maoni mengi yanaokena ni ya watanzania ambao wamo ndani ya tanzania ambao happana shaka ujio na uamuzi wa kujitolea muhanga wa kulitumikia taifa wa ndugu Fernandes ni msaada mkubwa wa maisha yao pia. Kwa kweli inasikitisha kuona watanzania kukosa uzalendo kiasi cha kutia aibu. kwanza kama karudi kweli kwa zamira ya kizalendo na kuwa mfano kwa wale watanzania walio na uwezo wa kulisaidia taifa lakini wakapotoka badala yakuweka maslahi ya taifa kwanza wanafikiria ubinafsi na umimi kwanza basi Mungu atamuezesha kufikia malengo yake . Pili mazingira ya utawala wa serikali ya awamu ya tano hayatofautiani kabisa na mazingira ya kazi ya serikali za nje hasa katika masuala ya midhamu na uwajibikaji. Na tatu tunaimani huyu kijana hatakuwa na ajenda za siri katika nia yake ya kulitumikia taifa kwani kuna mifano mingi ya wasomi wengi katika mataifa tofauti waliosoma Marekani kuwa na tabia ya ndume la kuwili. Sio siri ukachero uwe wa kisiasa, kibiashara, kidini, kiteknolojia nakadhalika ndiko kulipolipaisha taifa la Marekani kimaendeleo na kwa kweli ni wazuri mno kwenye fani hiyo kiasi cha kutengeza viongozi wa mataifa mengine kuwa viongozi wa Marekani kwa maslahi ya Marekani wakati mwengine bila ya hata ya hao viongozi kujua yakwamba wanaitumikia Marekani kwa maslahi ya Marekani kupitia nchi zao.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ni kipi ambacho huyo ndugu atakileta hapa nyumbani, km ni wasomi kwa sasa tanzania ina ziada ya wasomi ktk kila kada, hapo uzalendo siuoni kwani yeye alishapata fursa huko nje, kurudi nyumbani ni kuja kuwabana ndugu zake waliopo huku nyumbani kwani atachukuwa nafasi ya mtanzania mwenzake ambae hajabahatika kupata nafasi ya kutumika nje ya nchi, alipaswa aitumie fursa ya ajira nje ya nchi kwa kukusanya mtaji na kuja kuwekeza nyumbani, na sio kukimbilia nyumbani kuja kuwakaba wengine ambao wamehitimu vyuo na bado wanahangaika na bahasha mikononi, hapo hakuna uzalendo ndugu,

      Delete
    2. Hivi unaelewa kweli? usomi sio vyeti ni jinsi utakavyoweza kutumia elimu na akili yako kusonga mbele. Hao unaosema wamejaa ni wasomi wa vyeti wanaosubiri kuajiliwa, it appears you are one of them. Kwa profile yake huyo kijana siyo wa kubezwa.

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad