Mtoto wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, marehemu Upendo Msuya amesema, kujiuzulu kwa mama yake kulitokana na kuugua kwa muda mrefu kulikosababisha akate kauli tangu Oktoba mwaka jana.
Masha Msuya, mtoto wa pili wa Jaji Msuya, alisema hali ya mama yake ilizidi kuwa mbaya mara baada ya kurudi kutoka India alikokuwa akitibiwa Oktoba mwaka jana.
Jaji huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi katika Hospitali ya Kairuki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
“Mara ya mwisho sisi kuongea na mama vizuri ni mwezi wa 10 mwaka jana na muda wote huo mama alikuwa anawasiliana na sisi kwa kutumia maandishi,” alisema Masha.
Kabla ya kifo chake, Mei mwaka huu Msuya pamoja na Jaji Aloysius Mujulizi waliomba kujiuzulu nyadhifa zao, kitendo ambacho Rais John Magufuli alikiridhia.
Baada ya kujiuzulu taarifa mbalimbali zilizagaa zikidai kuwa Jaji Msuya alijiuzulu kwa sababu ya kutotenda haki katika kesi za dawa za kulevya alizozitolea hukumu.
Hata hivyo, Masha alisema mama yake alikuwa amekata kauli na hicho ndicho kilichokuwa chanzo cha kujiuzulu nafasi hiyo.
Alisema mama yake alisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu ambalo lilikuwa likijirudia mara kwa mara, hali iliyomsababishia ugonjwa wa kiharusi na kumfanya kutokuwa na uwezo wa kuongea vizuri.
Alisema mwaka huu ndio ulikuwa muda wa mama yake kustaafu na alipewa uhamisho kutoka Tanga kuja Dar es Salaam na ndipo alipowaambia watoto wake kuwa anataka kuandika barua ya kustaafu.
Alisema hiyo ndiyo moja ya sababu ya kujiuzulu kwa mama yake kwa kuwa kwa kazi yake ya ilihitaji kuwa na uwezo wa kuzungumza.
“Tutamkumbuka daima pamoja na kwamba alikuwa hawezi kuongea wala kutembea kutokana na ugonjwa wa kiharusi, lakini alikuwa anasisitiza upendo kwetu kila mara na yote hayo aliyafanya kwa kuandika,” alisema.
Mume wa marehemu, Hilary Msuya alisema kuondoka kwa mkewe ni pigo kwao, kwani afamilia ilikuwa inamtegemea kama mama.
“Kwa mapenzi ya Mungu ametutoka tukiwa bado tunamhitaji,” alisema Msuya.
Msuya alisema viongozi waliofika kutoa pole ni pamoja na Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta.
Majaji wengine waliofika kwenye msiba huo ni Richard Mziray, Sekieti Kihio na Pellagia Khaday.
Alisema, ibada ya kuaga mwili wa Jaji Msuya itafanyika Jumamosi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Wazo Hill na mazishi yatafanyika katika makaburi ya Kinondoni.
Jaji Msuya aliteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Mei 28 2008 kushika wadhifa huo akiwa pamoja na majaji wengine kumi na moja.