Watu wasiojulikana wameshambulia nyumba ya mashambani ya naibu wa rais wa Kenya William Ruto magharibi mwa Uasin Gishu kaunti, ripoti zinasema.
Ripoti katika eneo hilo zinasema kuwa washambuliaji hao waliwashinda nvguvu polisi mmoja katika lango la nyumba hiyo na kuingi ndani.
Ufyatulianaji wa risasi uliendelea katika nyumba hiyo ambayo imezungukwa na maafisa wa polisi.
Bwana Ruto hakuwepo nyumbani wakati huo.
Kisa hicho kinajiri siku 10 kabla ya Kenya kufanya uchaguzi wa urais , ubunge na ule wa kijimbo.
Naibu wa rais alikuwa ameondoka saa chache kabla ya uvamizi huo ili kuhudhuria mkutano wa kampeni katika mji wa Kitale, ambapo alijiunga na rais Uhuru Kenyatta.
Kenyatta anatetea kiti chake cha urais mwezi ujao, Huku uchaguzi wa 2013 ukifanyika kwa njia ya amani kulikuwa na ghasia mbaya za baada ya uchaguzi 2007 ambazo zilisababisha vifo vya watu 1000 huku wengine 600,000 wakiwachwa bila makao.
Hatahivyo wataalam wanasema hawatarajii kuona kiwango cha ghasia kama hicho kufuatia uchaguzi wa Agosti 8.