Siku moja kabla ya mdahalo wa wagombea urais, Rais Uhuru Kenyatta ambaye timu yake inasema hatashiriki alijichanganya na mashabiki wake wa Facebook kwa kujibu maswali waliyomuuliza.
Tukio hilo lilikuwa kubwa na lilionyeshwa mubashara kupitia vituo vya televisheni vya KBC na K24 TV.
Akiwa amevalia fulana, mkuu huyo wa nchi alijibu maswali mbalimbali ya wafuasi wake aliyokuwa ametumiwa mapema tena yale ambayo yeye na timu yake walichagua. Maswali hayo yaligusia nyanja za uchumi, rushwa, uchaguzi ujao na maendeleo ya miundombinu.
Katika majibu yake Kenyatta aliwataka mashabiki na wafuasi wake wapatao milioni 3 kuombea amani uchaguzi na kwa unyenyekevu aliomba achaguliwe kwa muhula mwingine wa kuwaongoza Wakenya.
“Ni lazima tupendane,” alisema moja kwa moja kutoka Ikulu ya Nairobi. “Na ujumbe huu ninaoutoa Jumapili hii wakati wengine wako kanisani, nawasihi muombe: Kwamba tutaishi kwa Neno. Kwamba tunapendana.”
Akitambua kwamba asilimia 51 ya Wakenya 19.6 milioni waliojiandikisha kupiga kura wana umri kati ya miaka 18 na 35, Rais Kenyatta aliyajenga maswali yake na kwa ukweli maswali aliyochagua kuwaridhisha vijana na kwamba Serikali inayoundwa na yeye ndiyo bora kwa ajili yao.
Katika kujibu maswali hayo alielezea maendeleo ya nchi kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, usambazaji umeme na matarajio ya kuongeza ajira kwa vijana.
“Tuna mpango wa kujenga mtandao wa reli jijini Nairobi, kupanua reli ya SGR hadi Naivasha na Narok, kisha ipite Kisumu,” alisema kwa watumiaji wa Facebook.
“Hatujachelewa tuko kwa wakati,” alisema na akatetea mapambano dhidi ya ufisadi akisema Serikali yake haitawavumilia kamwe.