Sababu za Ngeleja Kurejesha Fedha zabainishwa

MBUNGE wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja amesema moja ya sababu za kurudisha fedha za mgawo wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni kugundua aliyempa fedha hizo, amehusishwa na kashfa ya kuzipata kinyume cha sheria.

Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini, amerudisha serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Sh milioni 40.4 alizopewa kama msaada na mfanyabiashara James Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd ya Dar es Salaam. Aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba alipokea fedha hizo bila kujua kuwa zilikuwa zinahusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow kama ilivyo sasa.

Alisema fedha hizo alizipokea kwa nia njema kama msaada au mchango ili zimsaidie katika kutimiza majukumu yake ya kibunge hususan kusaidiana na wananchi wa jimbo lake kutekeleza shughuli za kijamii ikiwemo kujenga misikiti, makanisa na kusaidia wanafunzi wasiojiweza na kusaidia miradi ya maendeleo ambayo haipo kwenye Bajeti ya Serikali.

“Fomu ya tamko langu kama kiongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995 kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2014 niliyoiwasilisha ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Desemba 24, 2014 ilijumuisha msaada huu,” alieleza. Aidha, Ngeleja alisema Januari 15, 2015 alilipa kodi kwa TRA kiasi cha Sh 13,138,125 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya msaada huo aliopewa kama ilivyoelekezwa na TRA.

“Nilipokea msaada huu kama wapokeavyo wabunge wengine kwa nia njema, bila kujua kwamba Rugemalira baadaye angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha za akaunti ya Escrow kama ilivyo sasa,” alisema Ngeleja akirejea kufikishwa mahakamani mwezi uliopita kwa Rugemalira na mshirika wake wa kibiashara, Habinder Sethi wakihusishwa na utakatishaji wa fedha hizo zilizotokana na Akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema ameamua kurudisha fedha hizo, kwa kuwa imedhihirika kwamba aliyempa msaada anatuhumiwa kwenye kashfa ya akaunti ya Escrow, hivyo amepima na kutafakari na hatimaye kuamua kwa hiari yake kurejesha fedha hizo serikalini bila kujali kwamba alishazilipia kodi ya mapato. “Nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa tu, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa na tuhuma hizi,” alieleza mbunge huyo na kuongeza: “Nina zaidi ya miaka kumi na miwili nikiwa kiongozi wa umma na pia niliwahi kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini… lakini sijawahi kukumbwa na kashfa ya rushwa au ufisadi.

Kwa hiyo nimesononeka na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma.” Ngeleja alisema, “nimerudisha fedha hizi ili kulinda heshima na maslahi ya nchi yangu, chama changu CCM, serikali yangu, jimbo langu la Sengerema, familia yangu na heshima yangu mwenyewe.” Alisema kupokea msaada ni jambo la kawaida, ila ikibainika msaada unaopewa una harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo husika ni vyema kujiepusha nao.

Pia alimpongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa maslahi ya Taifa na kwamba anaungana na Watanzania wazalendo kumuombea kwa Mungu na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa kupigania maendeleo ya nchi. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu suala la makinikia, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kina kwa kuwa lipo katika uchunguzi kwa sasa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad