Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Chama Cha Wananchi CUF Dar es Salaam, wameunga mkono operesheni ya kuwaondoa wasaliti wa chama hicho waliopo ofisi kuu za chama hicho Buguruni.
Operesheni hiyo ilitangazwa wiki chache zilizopita na mbunge wa Ubungo, Said Kubenea ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Pwani.
Wakizungumza na waandishi wa habari wenyeviti hao wamesema watahakikisha wavamizi wanaondoka kama walivyoingia kwenye ofisi hizo.
Akitoa tamko kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtambani, Bakari Kasubi amewataka wanachama na viongozi wa CUF kujiandaa kukabiliana na mfumo kandamizi wa demokrasia nchini.
"Tunatakiwa kukabiliana na mfumo kandamizi na kuwashughulikia vibaraka wote kwa namna inavyostahiki,"amesema.
Kasubi amesema: "Wenyeviti wote wa Cuf tunapinga vikali njama na mipango ya msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi kwa kujiingiza kwenye vitendo vinavyolenga kuivuruga taasisi yetu."