Ukweli wa Simba Kumnyonyesha Mtoto wa chui Ngorongoro Wajulikana....

SIKU mbili tu baada ya kusambaa mitandaoni kwa picha ya tukio nadra la mama simba kumnyonyesha maziwa kwa upendo mtoto wa chui kwenye Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha, hatimaye undani wa jambo hilo umepata ufafanuzi wake.

Juzi, habari iliyoambatana na picha ya tukio hilo, ambalo kwa mara ya kwanza lilirushwa na Shirika la Habari Uingereza (BBC), ilitawala katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuibua mjadala. Mtoto wa chui alionekana akimnyonya maziwa mama Simba ambaye naye, alionyesha ukarimu mkubwa kwa kuketi chini pasi na hofu yoyote.

Picha hiyo ilipigwa na Joop Van Der Linde, mgeni aliyekuwa katika eneo la Ndutu Safari Lodge, Tanzania. Aidha, taarifa zilizorushwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, zilieleza kuwa simba huyo mwenye miaka mitano amewekewa mfumo wa ufuatiliaji (GPS) katika shingo yake ili kutambua mwenendo wake.

Katika mahojiano na Nipashe, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi, alisema kitendo cha simba huyo aitwaye Nosikitok kukutwa akimnyonyesha mtoto wa chui siyo kitu cha ajabu kwa wataalamu wa masuala ya wanyama kwa sababu hao (simba na chui), wako kwenye jamii moja.

Akieleza zaidi, Dk. Manongi alisema simba na chui si maadui kwa kuwa wako kwenye ikolojia tofauti na huwa hawadhuriani katika harakati za kusaka milo yao.

Alisema wanyama hao ambao walionekana wakinyonyeshana Jumanne (Julai 11, 2017), wana tofauti katika malisho yao na pia namna ya uwindaji, hiyo ikiwa ni sababu mojawapo kubwa ya kutopigana bali kusaidiana.

Akisimulia kuhusu simba huyo, Manongi alisema alizaa mwishoni mwa Juni mwaka huu, lakini inawezekana watoto wake hawapo kwa sasa.

TABIA ZA SIMBA, CHUITaarifa zaidi za kitaalamu zinaeleza kuwa simba na chui ni wanyama walio katika kundi la mamalia, yaani wanyama wanaonyonyesha na wako katika ukoo wa paka na wana maumbile yanayofanana na paka.

Simba ni miongoni mwa jamii ya paka wakubwa, akiwa ni wa pili kwa ukubwa nyuma ya chui.

Chakula cha simba ni nyama kama ilivyo kwa chui na wote wamekuwa wakiwinda wanyama lakini wao kwa wao hawadhuriani.

Simba hutegemea chakula kwa kuwinda wanyama wadogo na hata wakubwa na wakati akiwa mawindoni, huwinda kwa kunyatia na anapokaribia windo lake ndipo huchomoka kwa kasi. Mara nyingi simba jike ndiye muwindaji mzuri kuliko dume.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ukweli wenyewe uko wapi?Naona unajiuma uma tu story haiekeweki simba na chui wanakula nyama ba mambo kibao bla bla bla sababu yenyewe hasa kama kisemavyo kichwa habari yako magumashu hakieleweki duh uandishi wa habari wa kibongo bongo bana yaani bado safari ndefu kweli kweli siyo mchezo

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad