Mchezaji wa klabu ya Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Simon Msuva sasa yupo tayari kwenda kuanza maisha mapya ya soka la kulipwa nje ya Tanzania na hii ikiwa ni mara yake ya kwanza.
Kiungo huyo muhimu wa Yanga SC anakwenda nchini Morocco kujiunga na timu ambayo imeridhia kuwalipa wana jangwani hao kiasi cha dola 80,000 (Sh milioni 177) kwa kandarasi ya miaka mitatu.
Kupatikana kwa fedha hizo kutaifanya klabu hiyo kufanya usajili wa uhakika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.
Klabu hiyo iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita, imekubali kumlipa Msuva mshahara wa dola 4,000 (takribani Sh milioni 9).
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Msuva ameamua kujiunga na Klabu ya Difaa al Jadida ya Morocco ambayo imekuwa ikimuwania kwa takribani miezi mitatu sasa.