Wabunge 10 na madiwani wawili walioitwa kwa ajili ya mahojiano leo katika ofisi za Chama cha Wananchi (CUF) hadi saa 5.00 walikuwa bado hawajaonekana kwenye ofisi hizo.
Wabunge hao wanaomuunga mkono, Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad waliitwa ili kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho kuhusu mgogoro unaoendelea.
Katika taarifa iliyotolewa jana na chama hicho upande unaomuunga mkono, Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba uliwataka viongozi hao kufika katika ofisi hizo saa 3.00 asubuhi leo.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwepo katika ofisi hizo hakuwaona wabunge wala madiwani hao kwenye ofisi hizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mbunge wa viti maalum wa chama hicho aliyeitwa kwenye mahojiano hayo, Severina Mwijage amesema hana taarifa za kuitwa kwenye kikao hicho.
“Niko safarini Bukoba sifahamu kuhusu kuwepo kwa kikao hicho,” amesema.
Mbunge mwingine wa viti maalum wa chama hicho, Mgeni Kadika alisema alipata taarifa za kuwepo kwa kikao hicho lakini hatahudhuria.
“Nilipata taarifa kupitia ujumbe mfupi (SMS) lakini sitafika kwenye kikao hicho kwa kuwa nauguliwa na watoto huku Pemba," amesema.