Mkutano wa saba uliomalizika mjini hapa wiki iliyopita, haukuacha rekodi ya kufanya mabadiliko makubwa katika Bajeti Kuu ya Serikali pekee, bali pia baadhi ya wabunge kuacha gumzo kutokana na hoja na mambo yao.
Mkutano huo ulioanza Aprili 4 na kumalizika Jumatano iliyopita, ulipitisha bajeti ya Sh31.7 trilioni iliyokuwa na nafuu kwa wamiliki wa magari, wamiliki wa malori lakini pia kuuma kwa upande mwingine, huku likipitisha sheria mpya za usimamizi wa madini zitakazofumua mikataba ya sasa inayoonekana kuwa ni ya kinyonyaji.
Ili yote hayo yatokee, ilikuwa ni lazima wabunge washiriki katika mijadala na hapo ndipo kila mmoja aliacha nyayo zake.
Miongoni mwa wabunge ambao walitikisa kwa hoja zao kuvutia, kufikirisha au kuwachoma wengine ni Joseph Msukuma (Geita Vijijini), John Mnyika (Kibamba), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Halima Mdee (Kawe), kwa mujibu wa mwandishi wetu, Sharon Sauwa aliyeripoti shughuli za Bunge la Bajeti kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Wengine ni Philipo Mulugo (Songwe), Salma Kikwete (kuteuliwa), Mwita Waitara (Ukonga) na Hussein Bashe (Nzega Mjini).
Kiboko yao alikuwa Msukuma kwa jinsi alivyowachachafya baadhi ya mawaziri kila alipokuwa akitoa michango yake kwenye bajeti mbalimbali. Alidiriki kutaka baadhi ya mawaziri wafanyiwe usaili kabla ya kupewa nafasi hizo ambazo hutokana na uteuzi wa Rais.
Pamoja na kuwashambulia mawaziri, alipongeza ripoti mbili za kamati zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini ya dhahabu na kuwataka wenzake wawe jasiri, akiwataja makada wa CCM ambao wapo bungeni.
“Tufike mahali tuambiane ukweli tuache mizaha, tumeangalia (ripoti) watu wote. Maprofesa, watu tusiosoma na wananchi wetu kule vijijini, halafu wabunge mliotajwa kutoka CCM mnaanza kuweka kwenye Twiter (mtandao) mimi sihojiwi mpaka nini?” alihoji Msukuma, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM mkoani Geita.
“Hivi kweli wezi wana kinga gani? Kama kweli wametajwa ni wezi hata kama wapo CCM hili sio suala la mizaha. Kuna maisha ya watu na watu tumeumia. Watu mmetajwa, wabunge wenzangu wa CCM humu halafu mzee wetu tunayemheshimu humu ndani anasema hawezi kuhojiwa mpaka mahakamani yeye ni nani?
“Naomba kama kuna uwezekano hawa watu kama ni mbunge, kama ni nani wakamatwe. Wanaotusumbua humu ndani ni hao hao wametajwa kwa Profesa (Nehemiah) Ossoro. Katajwa (Dalaly) Kafumu, (William) Ngeleja na (Andrew) Chenge.
“Wana kinga gani kama ni wezi? Kwani magereza imewekwa kwa ajili ya kina Babu Seya peke yao? Tufike mahala tulipiganie Taifa hili, CCM si kichaka cha wezi. Kila mwaka kila tuhuma mtu anatajwa tufike mahali tuwe serious (makini) kwenye suala hili.”
Wakati Msukuma akitaka wachukuliwe hatua, Mnyika yeye alijikitika kwenye miswada ya rasilimali za nchi ambayo iliwasilishwa kwa hati ya dharura.
Alinukuu kauli ya Msigwa aliyoitoa bungeni mwaka 2012 kuwa Bunge dhaifu huzaa Serikali dhaifu.
“Kinyume chake, Serikali dhaifu husababisha Bunge kuwa dhaifu na ndio hali tuliyonayo hivi sasa. Bunge letu limefanywa dhaifu sana,” alisema Mnyika.
“Wakati Bunge lenye nguvu lingesema leo tunajadili mkabata huu na kesho mkataba huu, kwa udhaifu huu wa Bunge unaoendelea, tunaijadili yote.”
Kauli hiyo ilimfanya Spika Job Ndugai aingilie kati na kumjibu kuwa anayeona wenzake waliochaguliwa na wananchi kuwa ni dhaifu, basi naye ana matatizo.
“Huwezi tu-- hivihivi una akili timamu-- halafu ukawaona wenzako wote kundi la wajinga fulani,” alisema.
Pia, katika mkutano huo, Mnyika alizua kizaazaa kilichosababisha atolewe nje alipotumbukiza suala la ripoti ya makinikia wakati akichangia moja ya bajeti za wizara.
Wakati akitoa mwongozo kwa mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde kuwa wapinzani hawatetei wezi bali dhahabu inaendelea kuibiwa licha ya Serikali kupiga marufuku usafirishwaji nje wa mchanga, sauti ilisikika ikimwita Mnyika kuwa mwizi.
Hapo ndipo alipochachamaa kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya mtu huyo, lakini Spika alikana na badala yake akamtoa nje.
Siku chache baadaye, Serikali ilitangaza kuanzisha kodi ya asilimia moja kwa dhahabu ambayo itakuwa ikisafirishwa nje.
Msigwa
Mbunge mwingine ambaye amekuwa akisisimua vikao vya Bunge ni Msigwa, ambaye safari hii aliiponda Serikali akisema tangu mwaka 1980 hadi 2010 nchi za Afrika pamoja na rasilimali ilizonazo zimepoteza dola 1.4 trilioni za Kimarekani 1.4 kutokana na uongozi mbovu.
“Katika Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na changamoto kubwa ambazo takwimu hizi zinashabihiana kuwa tutaendelea tena kupoteza mali tulizonazo kutokana na uongozi,” alisema mchungaji huyo wa Kanisa la Vineyard.
“Nchi yetu ipo katika giza kinene kwa sababu watu wengi wamepewa mamlaka kuamrisha, lakini wao wenyewe hawajawahi kujifunza namna ya utii. Tatizo kubwa tulilonalo ni poor leadership skills (stadi dhaifu za uongozi), ambayo inaweza kutupeleka kuingia katika matatizo makubwa sana.
“Wanadhani kumsifu Rais kila anachosema ni uzalendo. Tukifanya hivyo tunatengeneza Taifa la watu waoga. Tupo hapa kuwafanya viongozi wetu wawe wanawajibika na ndiyo wajibu wetu.”
Zitto
Zitto Kabwe, ambaye safari hii ameingia bungeni kwa tiketi ya ACT Wazalendo, ni miongoni mwa wabunge wanaoacha nyao kwa hoja zao. Safari hii, Zitto kiongozi aliyerejea ahadi ya Rais ya kumtua mama ndoo, kuwa haiendani na bajeti ya Wizara ya Maji ambayo fedha za maendeleo zimepungua kutoka Sh915 bilioni hadi Sh623 bilioni.
Alisema wabunge wana mamlaka na kanuni za Bunge zinawaruhusu kuitaka Serikali ikapange upya bajeti hiyo na njia moja tu ya kumsaidia waziri ni bajeti hiyo kuandikwa upya.
Mdee
Mdee pia alitikisa Bunge kwa matendo yake. Kwanza alishtakiwa kwa kumtolea Spika maneno yasiyofaa, lakini akaomba msamaha ulioonekana wa dhati na kusamehewa.
Baadaye, Halima na mbunge mwenzake wa Chadema, Ester Bulaya walifungiwa kwa mwaka mmoja kutokana na kuonyesha vitendo ambavyo Bunge liliviona ni vya ukiukwaji wa kanuni.
Wakati Mnyika akitolewa na askari wa Bunge kwa kutotii kiti cha Spika, Mdee aliwafuata askari hao na kujaribu kumvuta mmoja bila ya mafanikio.
Kwa kuwa wawili hao walishamaliza adhabu zote, Bunge liliamua kuwazuia kuhudhuria vikao kwa mwaka mzima.
Mulugo
Mulugo ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu, akichangia bajeti ya wizara hiyo alisema kitendo cha kuchapisha vitabu vyenye makosa kinaitia doa Serikali. Alisema watalaamu waliopo katika Taasisi ya Elimu Tanzania wanatakiwa kuangaliwa.
“Suala la vitabu unaweza ukalia, nimefanya uchunguzi wa vitabu ni hatari na aibu ya dunia kuna mambo mengine lazima tuseme Serikali ni ya kwangu, nchi ya kwangu, hatuwezi kufumbia macho.”
Waitara
Waitara, ambaye ni mbunge wa Ukonga (Chadema), aliamua kuwashambulia wabunge wa CCM kwa kile alichoikiona kuwa ni kuisaidia Serikali kujibu. Alikuwa akichangia muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017.
“Tunatarajia kama hoja tumetoa sisi (upinzani), waziri aje kujibu, sio wabunge wa CCM mnaijibia Serikali. Mwisho wake mawaziri wanashindwa kufanya kazi vizuri,” alisema Waitara.
Bashe
Hussein Bashe, mmoja wa wabunge walioingia kwa mara ya kwanza na ambao wameonekana kuwa na hoja nzito, alizungumza kwa uchungu wakati akizungumzia vitendo vya utekaji nyara watu vilivyojitokeza mapema mwaka huu.
Bashe alisema kuna wabunge 11 ambao wamo katika orodha ya kutekwa.
Alisema watu kadhaa wamekuwa wakitekwa akitoa mfano wa yeye mwenyewe, Msukuma, Adam Malima, Ben Saanane na msanii wa Bongo fleva Roma Mkatoliki na kutaka suala hilo lijadiliwe.
“Ni jambo la dharura kwa sababu hawa ni watu wanaofahamika. Hatujui ni Watanzania wangapi wasiofahamika katika ngazi za chini (wanaotekwa),” alisema Bashe.
“Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema jambo hili ni la dharura kwa sababu kikundi hiki kilichoko ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kilichoamua kuchukua mamlaka haya ya kuteka watu, kinaharibu heshima ya Serikali yetu.
“Kinaharibu heshima ya chama changu, ambacho mimi na wabunge wenzangu wa CCM tuliomba ridhaa ya kuwaongoza na si kuhatarisha maisha yao. Naibu Spika naomba uruhusu Bunge kujadili jambo hilo.”
“Hali ya nchi si salama. Watanzania wanataharuki. Watanzania wanajadili mambo hayo katika mtandao na hakuna kauli ya Serikali.”