Waliokuwa walinzi 28 wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia, wameshindwa kutoka ndani ya eneo la mgodi huo kwa siku nne mfululizo kuanzia Julai mosi, baada ya vitambulisho vyao vinavyotumika kufungulia milango kufutwa kwenye mfumo wa ulinzi.
Hatua ya kufuta vitambulisho vya walinzi hao ambao ajira zao zilikoma tangu Juni 30, kutokana na kampuni hiyo kufuta idara ya ulinzi na kukabidhi jukumu hilo kwa kampuni binafsi ya G4S, kunatokana na wao kugoma kusaini mikataba mipya wa kuajiriwa na kampuni hiyo mpya.
Ingawa uongozi wa mgodi wa Buzwagi haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo licha ya awali, Meneja Rasilimali watu, Ivo Masanja kuahidi kulitolea ufafanuzi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhil Nkurlu alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.
Akizungumza ofisini kwake jana baada ya kuonana na walinzi hao, Nkurlu alisema Serikali ngazi ya wilaya na uongozi wa mgodi wamekubaliana walinzi hao waendelee kupata huduma zote muhimu ikiwamo chakula ambazo awali zilizuiwa. Alisema katika msafara wake uliohusisha maofisa kutoka idara ya kazi, alisikiliza maoni ya walinzi na uongozi wa mgodi na kubaini uhalali wa kampuni hiyo ya kuchimba madini wa kukabidhi jukumu la ulinzi kwa kampuni binafsi, lakini akaushauri uongozi kuendelea kuwahudumia waliokuwa watumishi hao hadi suala lao litakapopatiwa ufumbuzi kwenye baraza la ushuluhishi, Julai 10.
“Pia, tumekubaliana na hoja ya walinzi kuwa walikuwa na haki ya kugoma kusaini mkataba mipya kwa sababu suala hilo liko kwenye mchakato wa majadiliano yanayotarajiwa kukamilika Julai 10,” alisema Nkurlu.
Akizungumzia sakata la walinzi hao, Ofisa Uhamasishaji Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Nishati Tanzania (Numet), Shigela Aloyce alisema chama hicho kimekuwa kikifuatilia suala hilo bila mafanikio, kabla ya kuamua kulifikisha baraza la usuluhishi kwa uamuzi.
Mgodi huo ulikuwa na walinzi 107, kati yao, 52 walikubali mabadiliko na kusaini mkataba wa ajira kwenye kampuni mpya, 28 waligoma huku wengine 27 waliokuwa likizo nao wakijikuta vitambulisho vyao havina kazi.
Alipopigiwa simu jana ili kuzungumzia suala hilo, Msemaji wa Acacia, Nector Foya aliahidi kutoa majibu ifikapo saa 6:00 mchana ahadi ambayo hakuitekeleza hadi saa 11:00 jioni baada ya kudai kuwa yuko kwenye kikao.