Wanaume watatu ambao walimvamia, wakamvua nguo na kumuibia mwanamke ndani ya basi la abiria mjini Nairobi, katika kisa ambacho kilirekodiwa na kusambazwa pakubwa katika mitandao ya kijamii miaka mitatu iliyopita, wamehukumiwa kifo kwenye mahakama moja mjini Nairobi.
Hukumu hiyo ya kifo ilitolewa baada ya watatu hao kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia nguvu.
Kifungo kingine cha miaka 25 kilitolewa kwa kumvua nguo mwanamke huyo, Jilo Kadida.
Kifungo cha miaka 25 hata hivyo kilitupiliwa mbali kwa wanaume hao walikuwa tayari wamehukumiwa kifo.
Wanaume hao watatu ni dereva wa basi Nicholas Mwangi, na makondakta wake Meshack Mwangi na Edward Ndung'u.
Hakimu wa Nairobi Francis Andayi, alisema kuwa kitendo hicho kilikuwa kibaya walichoonekana kufurahia, kwa sababu walikuwa wakishangilia huku wakimvua nguo mwanamke huyo.
Muathiriwa aliiambia mahakama kuwa kulikuwa na karibu wanaume saba ndani ya basi wakati huo, ambao walitaka kumbaka lakini akadanganya kuwa alikuwa na vurusi vya ukiwmi, Video hiyo ilizua maandamano huku mamia ya wanawake wakishiriki maandamano mjini Nairobi.