WANAWAKE Waliotekwa na Kuolewa na BOKO HARAM Wataka Kurudi Kwa Wapiganaji Hao.....


Habari zilipoenea kuhusu baadhi ya wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa na wapiganaji wa kundi la Boko Haram mwaka 2014 kukataa kurejea nyumbani na wenzao walioachiwa kwenye kundi la 82 lililoachwa huru mwezi Mei, dunia nzima haikuamini kwamba jambo hilo lingeweza kutokea.
Video iliyotolewa na wapiganaji wa Boko Haram ikiwaonesha wanawake na wasichana walioshika bunduki wakisema kuwa wanafurahia maisha yao mapya haikutosha kuwaaminisha watu. “Itakuwa wamelazimishwa tu,” baadhi ya watu walikuwa wakisema. Nini zaidi ya hicho kitamfanya msichana au mwanamke yeyote kuamua kubaki na wanaume wa aina hiyo? Ndio swali kubwa lililowasumbua wengi.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake waliookolewa na majeshi ya Serikali ya Naijeria wamekuwa tayari kurudi kwa wapiganaji wa Boko Haram waliopo kwenye msitu wa Sambisa kwa hiyari yao wenyewe.
Mwezi Januari, muandishi wa BBC alikutana na kuzungumza na Aisha Yerima (25) ambaye alitekwa na wapiganaji hao zaidi ya miaka minne iliyopita. Alipokuwa huko, aliolewa na kamanda mmoja wapo ambaye alikuwa akimpenda sana na kumpatia zawadi za gharama na kumuimbia nyimbo za mapenzi za Kiarabu.

Amesema kwamba maisha haya mazuri aliyokuwa akiishi msituni yalikatishwa kwa kutokea kwa majeshi ya Naijeria mwanzoni mwa mwaka 2016 wakati mumewe alikuwa amekwenda kwenye mapigano akiwa na makamanda wenzake.

Mwandishi alipofanya mahojiano na Aisha kwa mara ya kwanza ilikuwa mwanamke huyo alipokuwa polisi kwa zaidi ya saa nane, na kumaliza programu ya kumfanya asiwe na msimamo mkali aliotoka nao porini aliyokuwa akifanyiwa na mwanasaikolojia Fatima Akilu, muanzilishi wa programu hii.
“Kwa sasa naona kabisa kwamba vitu vyote ambavyo tuliambiwa na Boko Haram ilikuwa ni uongo. Sasa hivi nikiwa nawasikia redioni najikuta nacheka,” alisema Aisha.
Wanavutiwa na madaraka waliyokuwa nayo?

Lakini ilipofikia mwezi Mei ikiwa ni chini ya miezi mitano toka awe huru na kuanza kuishi na wazazi wake jijini Maiduguri, Aisha alitoroka na kukimbilia msituni yalipo maficho ya Boko Haram.
Kwa miaka mitano iliyopita, Dkt. Akilu amekuwa akifanya kazi na waliokuwa wafuasi wa kundi la Boko Haram – wakiwamo baadhi wa makamanda, wake na watoto za – na mamia ya wanawake waliookolewa kutoka kwenye himaya yao.

“Ni jinsi gani wanawake walivyokuwa wanafanyiwa walipokuwa mikononi mwa Boko Haram inategemea walikuwa wameshikiliwa kwenye kambi ipi. Inategemea kamanda gani alikuwa anaongoza kambi hiyo,” alisema.

“Kwa wale waliokuwa wakiishi vizuri ndio waliridhia kuolewa na viongozi na wafuasi wa Boko Haram au wale waliojiunga na wapiganaji hao kwa kujitolea, ambao ndio wengi sana. Wanawake wengi hawakuwa wakipata matunzo sawa.”

Aisha alijisifu kwa mwandishi kuwa alikuwa na idadi kubwa ya watumwa alipokuwa kwenye msitu wa Sambisa, heshima kubwa aliyokuwa akiipata kutoka kwa makamanda wengine wa Boko Haram na nguvu kubwa ya ushawishi aliyokuwa nayo juu ya mumewe. Na alijisifu kuwa mara moja alimsindikiza na kwenda naye mpaka kwenye uwanja wa mapambano.

“Hawa ni wanawake ambao kwa muda mwingi hawajawahi kufanya kazi, hawakuwa na mamlaka yoyote, hawakuwa na sauti kwenye jamii, na mara inatokea wanakuwa na madaraka ya kuongoza wanawake kati ya 30 na 100 ambao sasa wanakuwa moja kwa moja watumwa wao wakitumwa na kufanya lolote watakaloambiwa,” aliongeza Dkt. Akilu.

“Ni ngumu sana kujua ubadilishe vipi hali hiyo ukisharudi kwenye jamii kutoka ulipokuwa mateka kwa sababu wengi wa wanawake hao wanarudi kwenye jamii ambapo hawataweza tena kuwa na mamlaka waliyokuwa nayo kabla ya kuokolewa.”
Bado mshangao ni mkubwa

Mbali na kutokuwa na mamlaka tena, sababu nyingine ambayo Dkt. Akilu anaamini inaweza kufanya wanawake hao kuwa tayari kurudi kwa Boko Haram ni pamoja na kutengwa na jamii inayowaona kama ni miongoni mwa wapiganaji hao tu kwakuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na hali ngumu ya kiuchumi wanayoipata wakiwa kwenye jamii ambayo hawawezi kuipata wakiwa na Boko Haram.

“Kuwaondoa misimamo mikali waliyojengewa ni jambo moja. Kuwafanya waweze kuishi kwenye jamii ni jambo la pili kwenye programu hii. Baadhi yao hawana watu wa kuwafanya wajisikie salama kuishi nao. Mara nyingi wanafanikiwa kuondoa misimamo yao mikali lakini wanapata tabu kuishi kwenye jamii na ni tabu inayowapelekea mara nyingi kujikuta wanarudi,” amesema Dkt. Akilu.
Mama wa Aisha amesema kuwa anakumbuka wanawake angalau saba ambao waliolewa na Boko Haram ambao wote walikuwa ni marafiki wa mwanaye walisharudi kwenye msitu wa Sambisa muda mrefu kabla ya Aisha.

“Kila mara mmoja wao alipotoweka, familia yake walikuwa wanakuja kwetu na kumuuliza kama Aisha kama wamewasiliana na mtoto wao,” alisema. “Na hivyo ndio tulikuwa tunajua.”
Baadhi ya wanawake hao walikuwa wanawasiliana na Aisha baada ya kurudi kwa wapiganaji wa Boko Haram. Mdogo wake, Bintu, alisikia mazungumzo ya simu ya dada yake angalau mara mbili.
“Walikuwa wanamwambia arudi na aungane nao lakini alikuwa anakataa,” alisema Bintu. “Alikuwa anawaambia kwamba hataki tena kurudi.”

Tofauti na baadhi ya waliowahi kuwa “wake” wa Boko Haram niliowahi kukutana nao ambao labda wanaishi maisha magumu au wanakumbana na unyanyapaa, kwahiyo maisha ya Aisha yalikuwa ni kama yanajulikana yatakavyokuwa.

Alikuwa anapata pesa kutokana na biashara ya nguo, alikuwa akihudhuria matukio mbalimbali ya kijamii na mara nyingine huweka picha zake kwenye mitandao ya kijamii akiwa na wenzake.

“Nadhani wamaume kama watano hivi walitaka kumuona,” alisema mama Aisha, akimaanisha kwamba jamii ilishakubali kuishi vizuri na mwanaye, na kusema kuwa hii inaashiria kuwa mwanaye hakukumbwa kabisa na unyanyapaa kabisa kutoka kwenye jamii.

“Mmoja wa wanaume waliokuwa wanamtaka anaishi jijini Lagos. Aisha alikuwa anafikiria kuolewa kabisa,” alisema.

Lakini kila kitu kilibadilika alipopigiwa simu na rafiki zake waliorudi porini wakimwambia kwamba mumewe wa Boko Haram alikuwa na mwanamke mwingine ambaye alikuwa mpinzani wa Aisha alipokuwa porini.

Tangu siku hiyo, Aisha tuliyemzoea anayependa kukaa na watu hakuwa yeye tena. “Aliacha kutoka, kuongea na watu au kula,” alisema Bintu. “Alikuwa na hasira muda wote.”

Wiki mbili baadaye aliondoka nyumbani na hakurudi tena. Baadhi ya nguo zake hazipo. Simu zake hazipatikani. Aliondoka na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka miwili aliyopata na kamanda wa Boko Haram kwenye msitu wa Sambisa, lakini amemuacha mkubwa kwa aliyekuwa mumewe ambaye waliachana kabla hajatekwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad