Shirika rasmi la habari la serikali ya nchi hiyo- (APS), linasema kwamba mashabiki wa timu mbili za soka, walikabiliana baada ya mchuano wa soka uliochezewa katika uwanja wa michezo wa Demba Diop stadium, kumalizika.
Ukuta uliporomoka wakati ambapo idadi kubwa ya watu walipokuwa wakiondoka kwa kasi uwanjani.
Idadi kubwa mno ya watu wamejeruhiwa.
Kisa hicho kilitokea wakati wa fainali ya kuwania kombe la ligi kuu nchini humo, kati ya timu ya soka ya Stade de Mbour na Union Sportive Ouakam.
Mapigano yalianza kati ya mashabiki wa timu hizo mbili hasimu, hatua iliyowachochea maafisa wa polisi kuwarushia vitoa machozi. Hatua hiyo ilisababisha taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki ambao walianza kukimbia na kusababisha mkanyangano, na kuporomoka kwa ukuta.
Baadhi ya mashabiki walirusha kila aina ya vifaa yakiwemo mawe.
Picha zinazosambazwa mitandaoni, zinaonesha watu wakikurupuka na kujaribu kupanda juu ya ukuta mfupi, huku wakizungukwa na wingu kubwa wa moshi wa vitoa machozi.
Runinga ya taifa ya nchi hiyo, inasema kuwa, magari ya huduma za dharura na vikosi vya zima moto vilifika maeneo ya tukio hilo.