Waziri wa Uganda Apongeza Mabasi ya Mwendokasi Dar

WAZIRI wa Nchi anayeshughulikia Uchukuzi nchini Uganda, Bagiire Aggrey Henry, ameusifu Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kwa namna unavyosaidia kurahisisha huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam.

Pongezi hizo alizitoa juzi baada ya kutembelea na kupanda basi la kuanzia Kivukoni hadi Morocco, akisema mradi huo umesaidia kuondoa msongamano wa magari.

Waziri huyo wa Uganda ambaye aliongozana na ujumbe wa Serikali yake kuja nchini kutembelea na kujifunza kuhusu mradi huo, alisema wana mpango wa kuanzisha mfumo kama huo katika jiji la Kampala.“Tumefurahi kuuona mfumo wenu wa mabasi yaendayo haraka unavyofanya kazi. Nasi tukirudi Uganda tutaenda kutekeleza kile tulichokiona,” alisema Bagiire.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, alisema mradi wa BRT umekuwa kivutio kikubwa cha wageni, ndiyo maana viongozi hao kutoka Uganda waliomba kuutembelea.

Dk. Chamuriho alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam na watumiaji wa usafiri huo kuitunza miundombinu yake ili idumu na kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu kutoka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi John Shau, aliwashukuru wageni hao kutoka Uganda kwa kutembelea mradi huo.

Hivi karibuni Jiji la Dar es Salaam kupitia Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka, lilipata tuzo ya mwaka ya usafirishaji endelevu duniani.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad