Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linamsaka mtuhumiwa huyo, Emmy Kyando (40, mkazi wa Sai jijini Mbeya ambaye aliwafanyia kitendo hicho cha kinyama watu hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga, aliwataja wengine waliomwagiwa tindikali kuwa ni Loveness John (11), mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Sinde na Nancy Peter (5), wakazi wa Mtaa wa Mwanshinga, Kata ya Manga jijini Mbeya.
Walimwagiwa na kujeruhiwa na tindikali hiyo usoni, kifuani na mikononi Julai 19, mwaka huu saa tatu usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mpinga alisema Emmy anadaiwa kufanya kitendo hicho kutokana na wivu wa kimapenzi kwa kuwa ni mke mwenza wa mwathirika.
Mpinga alifafanua kuwa baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho alikimbia kusikojulikana na wasamaria wema waliwakuta waathirika wakiwa katika hali mbaya na kuwapeleka katika Hospitali ya Rufani ya Mbeya kwa ajili ya kupata matibabu.
Kamanda Mpinga alieleza kuwa juhudi za kumtafuta mtuhumiwa kwa kushirikiana na mume wa muathirika huyo aliyefahamika kwa jina la Lausi Kidagile ambaye naye ni mkazi wa Sae zinaendelea.
“Jeshi la Polisi linalaani vikali kitendo hicho na tunaomba mwananchi yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kumkamata mtuhumiwa atupatie ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Kamanda Mpinga.
Akizungumza na Nipashe kwa taabu akiwa wadi namba mbili katika Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya, muathirika wa tukio hilo, Vumilia Shangema, alisema mtuhumiwa alikuwa akimtolea lugha za vitisho mara kwa mara na aliahidi kuwa kuna siku atamjeruhi.
“Nikiwa njiani na wanangu ghafla nikaona mwanamke mmoja niliyemfahamu kwa jina la Emmy akinimwagia kitu usoni na sikuweza kuona tena, lakini nikakumbuka kuwa Emmy aliwahi kuniambia kuwa atanifanyizia huku akinitolea vitisho vikali vilivyotishia usalama wa maisha yangu,” alisema Shangema.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya, Goodlove Mbwanji, alithibitisha kuwapokea wagonjwa katika hali mbaya hususani mama wa watoto Shangema, akiwa ameharibika usoni na macho kutokuona kabisa huku mtoto Loveness akiendelea kupata matibabu na afya yake kuimarika pamoja na Nancy ambaye alitibiwa na kuruhusiwa.
Mbwanji alisema wanaendelea na matibabu kwa mama huyo na kwamba idara ya upasuaji pamoja na madaktari wengine bingwa wamemuwekea uangalizi mzuri ili apate matibabu stahiki.