Katibu Mkuu wa klabu ya Mabingwa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans, Charles Boniface Mkwasa amepatwa na kigumuzi kwa kushindwa kuzungumzia sakata la kuondoka kwa msaidizi Juma Mwambusi na kudai suala hilo lipo katika uongozi linashughulikiwa.
Mkwasa ameeleza hayo baada ya kuwepo tetesi kuwa mkataba Mwambusi umefikia tamati tangu tarehe 30, Juni mwaka huu kuitumikia klabu hiyo.
"Suala la Mwambusi lipo kwenye uongozi linafanyiwa kazi lakini kama mwenyewe amezungumza hilo anaondoka basi ameongea yeye mwenyewe lakini mimi najua suala lipo katika uongozi na siwezi lisemea mpaka litakapofanyiwa kazi", amesema Mkwasa.
Katika hatua nyingine, Mwambusi amenukuliwa akisema anaondoka katika timu hiyo kwa kuwa kuna mambo mengine binafsi amepanga kuyafanya.
“Mkataba wangu umeisha tangu Juni 30, naushukuru uongozi na wana Yanga wote, kwa misimu miwili tumefanya kwa mafanikio… Naondoka kwa roho safi… Msimu wa kwanza tumechukua makombe mawili, msimu wa pili nimefanya kazi na makocha wawili na tumefanikiwa kuchukua ubingwa ….Sitakuwa kwenye mpira, nitakuwa kwenye mambo binafsi, nahitaji kupumzika, ila msimu unaofuata ikiwezekana tunaweza kuonana tena,”amesema Mwambusi
Kocha huyo ambaye amedumu Yanga kwa misimu miwili akitokea Mbeya City, amewataka wana Yanga wote kuendelea kushirikiana ili kuongeza mafanikio zaidi.
Kwa upande mwingine, Mwambusi ametaja deni kubwa ambalo timu hiyo inalo ni kutwaa kombe la mabingwa barani Afrika, kwa kuwa ubingwa wa Tanzania hadi sasa siyo kitu kigeni tena kwao.