ACT Wazalendo Wafuata Nyayo za CHADEMA,Waazimia Kwenda Mhakamani Kupinga Amri ya Serikali

ACT Wazalendo Wafuata Nyayo za CHADEMA,Waazimia Kwenda Mhakamani Kupinga Amri ya Serikali
Chama cha ACT Wazalendo kitafuata nyayo za Chadema baada ya kupitisha azimio la kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga amri ya Serikali kuzuia mikutano ya hadhara na shughuli halali za vyama vya upinzani.

Azimio la ACT limefikiwa juzi katika Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa pili wa chama hicho.

Wajumbe wa mkutano huo wameazimia pia kumuandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakitaka atengue amri waliyoiita batili ya kuzuia mikutano ya hadhara na shughuli halali za vyama vya siasa.

Kupitishwa kwa azimio hilo ambalo ni sehemu ya maazimio manne ya chama hicho, ni sawa na kuunga mkono harakati zilizoanzishwa na Chadema iliyowahi kufungua kesi Mahakama Kuu.

“Maazimio haya yote yatapelekwa kwenye idara husika za chama kwa ajili ya utekelezaji mara moja. Pia, viongozi wa chama wa ngazi mbalimbali wataendelea kuipigania misingi ya haki na demokrasia,” alisema Ado Shaibu ambaye ni Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT, kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa jana.

Azimio lingine la mkutano huo ni kukemea vitendo vya baadhi ya wakuu wa wilaya, watendaji wengine wa Serikali na vyombo vya dola wanaowanyanyasa na kuwakandamiza watumishi wa umma na wananchi kwa jumla, bila sababu ya msingi ikiwamo kuwaweka hovyo mahabusu. “Wajumbe wametoa rai kwa wananchi kuwapinga watawala wanaokumbatia vitendo vya kibabe dhidi ya wananchi na kwa wale watakaopuuza wito wa kuzingatia matakwa ya kisheria na kiutu katika kutekeleza wajibu wao, watengwe na jamii na wanyimwe ushirikiano,” ilisema taarifa hiyo.

Pia, wajumbe walisema kuna viashiria vinavyoonyesha kuwa mwenendo wa kiuchumi na hali ya maisha ya watu inazidi kuwa mbaya. “Wakati Serikali inajinasibu kuhusu viwanda, mauzo ya bidhaa zitokanazo na viwanda kwenda nje ya nchi yameshuka. Mwaka unaoishia Mei, 2016, Tanzania iliuza nje bidhaa za viwanda za thamani ya Dola1.5 bilioni za Marekani (Sh3.3 bilioni) lakini mwaka unaoishia Mei, 2017 Tanzania imeuza nje bidhaa za viwanda za Dola 0.8 bilioni tu,” ilisema taarifa hiyo.

ACT imesema uagizaji wa bidhaa za chakula kutoka nje umeongezeka kwa asilimia 14 ndani ya mwaka mmoja wa Mei 2016 mpaka Mei 2017 kwa Tanzania kutumia Dola 480 milioni hali inayotafsiri utegemezi zaidi nje ya nchi katika manunuzi ya bidhaa.    


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad