Ada za Vyuo Vikuu Nchini Zashuka......


Agizo la Aprili 15 lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipoitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iachane na utaratibu wa sasa wa kuwapangia wanafunzi vyuo bali iwaachie wanafunzi wenyewe kazi ya kutafuta vyuo wanavyotaka kwenda kusoma limesababisha vyuo vingi nchini kushusha ada, labda lengo ikiwa ni kujiongezea idadi ya wanafunzi itakaowadahili kwakuwa wengi wao wanaweza wakachagua vyuo vingine endapo gharama za ada ya masomo itakuwa kubwa zaidi ya vyuo vingine.

Hatua hii ya kupunguza ada inaonekana kuwa ni habari njema kwa wazazi na wanafunzi wenyewe lakini yawezekana ikawa ni mwiba mkali kwa wamiliki wa vyuo vikuu nchini kwani sasa wanalazimika kuja na mbinu kadhaa kuhakikisha wanaweza kudahili wanafunzi wengi zaidi ili kuziba tofauti ya kipato watakachopoteza kutokana na wanafunzi ambao sasa wapo huru kujichagulia wanapotaka kwenda kusoma. Uamuzi huu wa kupunguza ada umesababisha athari kubwa kwa vyuo kwani mapato ya baadhi ya vyuo yamepungua hadi asilimia 25.

Baadhi ya mambo mengine yaliyochangia kushuka kwa mapato ya vyuo vikuu na taasisi za elimu nchini ni pamoja na kulazimika kuondoa gharama za uchukuaji fomu ambazo kwa sasa zinatolewa bure kwa waombaji wa nafasi ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi. Katika baadhi ya vyuo, sababu kubwa ya kupunguza ada imetajwa kuwa ni kuwaongezea fursa Watanzania wenye sifa za kujiunga zaidi na vyuo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.

Aprili 15 mwaka huu, Rais Dkt. John Magufuli alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) alisema kuwa utaratibu wa sasa wa kuwapangia vyuo wanafunzi unawachanganya wanafunzi na hivyo unapaswa kuachwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad