Imesema imetangaza ajira hizo, ili kupata watendaji wa vijiji watakaoziba mapengo ya waliofariki na walioachishwa kazi kutokana na kuwa na elimu ya darasa la saba.
Kibiti ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Pwani ambazo kwa miaka miwili iliyopita, zimekumbwa na mauaji ya viongozi wa ngazi mbalimbali, wakiwamo watendaji na wenyeviti wa vijiji.
Mauaji hayo yalikuwa yakitekelezwa na watu wasiofahamika, waliokuwa wakivamia nyumba za watendaji hao na kuwaua kwa kuwapiga risasi.
Wilaya nyingine za mkoa huo zilizokumbwa na mauaji hayo ni Rufiji na Mkuranga.
Aidha, kutokana na kushamiri kwa mauaji hayo na vitisho vilivyokuwa vikitolewa na wauaji, baadhi ya watendaji wa vijiji waliripotiwa kukimbia makazi yao wakihofu kuuawa.
Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Alvera Ndabagoye, alisema hali ya wilaya yake kwa sasa ni shwari.
Kutokana na kurejea kwa hali ya utulivu wilayani humo, Ndabagoye alisema wameona sasa kuna haja ya kutangaza nafasi za kazi 45 za watendaji wa vijiji.
Ushwari huo unatokana na juhudi za Jeshi la Polisi, mkuu wake Inspekta Generali (IGP) Simon Sirro, ambaye baada ya kuteuliwa amefanikiwa kukomesha mauaji hayo huku jeshi hilo likitangaza kuwaua watuhumiwa 13 wa mauaji hayo kwa mpigo katika shambulizi moja, na wengine kukimbia.
Akifafanua tangazo lake la ajira, Ndabagoye alisema: "Tumetangaza nafasi hizi, ili kuziba pengo la wale ambao wana elimu ya darasa la saba ambao wanatakiwa kupisha wenye elimu ya juu zaidi."
Alisema, pia nafasi hizo zinatokana na kuhitaji watendaji wa vijiji watakaoziba mapengo ya waliofariki.
Alisema mwombaji anatakiwa kuwa na ufaulu wa elimu ya kidato cha nne au sita, aliyehitimu mafunzo ya astashahada au cheti katika fani za utawala, sheria, elimu ya jamii, usimamizi wa fedha, maendeleo ya jamii au sayansi ya sanaa kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma au chuo chochote kinachotambuliwa na serikali.
Alisema miongoni mwa kazi ambazo watatakiwa kuzifanya ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaimarika.
Alisema mwisho wa kutuma maombi hayo ni Septemba 11, mwaka huu.
Mapema mwaka huu Katibu tawala wa Wilaya hiyo, Milongo Sanga, katika kikao cha robo mwaka cha baraza la madiwani, kilichokuwa kikijadili maendeleo ya wilaya hiyo, alisema watendaji wa vijiji vilivyoko wilayani Kibiti wamezikimbia ofisi zao kwa hofu ya mauaji, hivyo kusababisha shughuli mbalimbali za kijamii kukwama.
Katibu Tawala huyo aliwaondoa hofu watendaji hao, hata hivyo, na kuwataka warejee katika ofisi zao, ili kuendelea kutoa huduma kutokana na kuwapo na hali ya amani.
MATUKIO YA MAUAJI
Tangu mwaka 2015, kumekuwa na matukio ya mauaji ya viongozi na askari polisi mkoani Pwani.
Baadhi ya matukio ya kuuawa kwa viongozi mkoani humo ni la usiku wa kuamkia Juni 28, mwaka huu, ambalo viongozi wawili wilayani Kibiti waliuawa na kundi hilo kwa kupigwa risasi.
Waliouawa siku hiyo ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi, Maiko Nicholaus na Mtendaji wa Kijiji cha Mangwi kilichopo Kata ya Mchukwi wilayani humo. Katika tukio hilo, wauaji pia walichoma moto nyumba za viongozi hao na kutokomea kusikojulikana.
Mauaji hayo yalitokea ikiwa ni wiki tangu kuuawa kwa kupigwa risasi kwa askari wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa kazini katika kijiji cha Msafiri, Kata ya Bungu wilayani humo.
Mbali ya kuwaua askari hao, wauaji walichoma moto gari moja na pikipiki moja ya askari hao kisha kutokomea kusikojulikana.
Mei mwaka jana, matukio matatu yalitokea ambayo ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunga, Saidi Mbwana.
Oktoba aliuawa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambuga, Ally Milandu baada ya kuvamiwa na watu wanne waliomshambulia kwa kumpiga risasi.
Novemba wenyeviti wawili wa vitongoji vya Kijiji cha Nyambunda waliuawa kwa kupigwa risasi kabla ya kuuawa kwa mfanyabiashara Oswald Mrope ambaye alipigwa risasi mbele ya familia yake katika kitongoji cha Mkwandara, kilichopo Kijiji cha Nyambunga Januari mwaka huu.
Februari yalitokea matukio mawil; la kwanza likihusisha majambazi waliovamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga ambaye alifanikiwa kutoroka, lakini wahalifu hao walirejea na kuimwagia mafuta nyumba yake na kuichoma moto.
Tukio la pili katika mwezi huo ni la mauaji ya Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya na Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji Mapato ya Ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na mlinzi Rashid Mgamba ambao waliuawa kwa kupigwa risasi.
Machi Jeshi la Polisi liliripotiwa kuwaua watu watatu katika Daraja la Mkapa walipojaribu kukwepa vizuizi vitatu va barabara wakiwa na pikipiki likiwatuhumu kuwa sehemu ya kikundi kinachoendesha mauaji hayo.
Aprili askari nane waliokuwa kwenye gari la polisi wakitoka kubadilishana lindo na wenzao, walipofika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilayani Kibiti, walishambuliwa na majambazi na saba kati yao, waliuawa kwa risasi huku mmoja akijeruhiwa.
Mei viongozi wawili; kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale na aliyekuwa katibu wa chama hicho, Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Arife Mtulia waliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.