Alichopatia na Kukosea Rais Mgogoro wa Ruge na Paul Makonda...

Wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania mambo mengi yaliibuka na kufurahisha watu lakini mengine yaliwasikitisha na mengine kuibua mshangao mkubwa kwani hawakutarajia kama yangetokea.

Wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika Kijiji cha Chongoleani nje kidogo ya Jiji la Tanga, Rais Magufuli alieleza ni kwa namna gani bomba hilo litaweza kuzinufaisha nchi hizi mbili (Tanzania na Uganda), lakini pia nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Mbali na hilo, Rais Magufuli alivipongeza vikundi mbalimbali vya burudani vilivyotumbuiza katika sherehe hiyo vikiwepo vikundi vya kitamaduni na pia bongo fleva. Wakati akitoa pongezi hizo, alimuita jukwaani Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Wawili hawa walikuwa na msuguano wa muda mrefu kufuatia tuhuma (ni tuhuma kwa sababu mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtia mtu hatiani) zilizotolewa kuwa, alivamia ofisi za Clouds Media Group akiwa na Polisi wenye silaha na kushinikiza kurushwa kwa kipindi ambacho kwa mujibu wa Ruge, hakikuwa na uwiano kwani hakikushirikisha pande mbili wakati wa kukiandaa.

Kufuatia tukio hilo, vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa, taasisi na wanaharakati wa haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari, wanasiasa waliungana pamoja wakitaka Rais Magufuli amuwajibishe Makonda lakini pia sheria ichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na Makonda kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Hadi naandika makala hii, hakuna hatua hata moja iliyochukuliwa kufuatia madai hayo ambayo hadi leo yameacha vidonda kwenye baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya kiongozi huyo.

Baada ya Rais kuwaita jukwaani vijana hawa wawili, aliwataka washikane mikono na wafanye kazi pamoja. Rais aliamini kuwa kwa kufanya hivyo atakuwa amesuluhisha mgogoro wa pande hizo mbili na vijana hao wanaweza kushirikiana tena kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Lakini ambacho wengi wamekiona, ni kama vijana hao wameamriwa kushirikiana (ombi la mkubwa ni amri), bila kutatua kwa usahihi matatizo yaliyowatenganisha.

Tukichambua kwa ufupi kitendo kilichofanywa na Rais mbele ya kadamnasi, tunaweza kufikia hitimisho kwa upande mmoja kwamba, lengo la Rais lilikuwa jema na zuri kabisa. Lengo la Rais ni kutaka kuona vijana hao na wengine nchini wanashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwani huo ni msingi wa maendeleo. Hata wahenga walisema Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu. Kwa lengo hili la kuleta umoja wa kitaifa, Rais alifanya kitu sahihi, na anastahili kupongezwa.

Kwa upande mwingine, licha ya kuwa lengo lake lilikuwa ni sahihi na lenye kujaa nia njema, njia aliyotumia kulifikia lengo lake haikuwa sahihi.

Mgogoro uliokuwepo/uliopo kati ya Ruge na Makonda si mgogoro wa watu wawili tena kiasi kwamba unaweza ukawaita na kuwaweka katika chumba ukawapatanisha wao na mambo yakawa sawa. Mgogoro huo ulipofikia ulikuwa ni mgogoro wa jamii dhidi ya kiongozi, mgogoro wa taasisi dhidi ya kiongozi, mgogoro wa tasnia ya habari dhidi ya kiongozi.

Tuchambue kwa ufupi, kwanini tunaeleza kwamba kuwashikisha mikono watu hawa wawili kunaweza kusitoe suluhisho la kudumu kwenye mgogoro wao;

Wakati tukio hilo limetokea, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lililaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vingine vya habari kutoandika habari za Makonda wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo ingekuwa ni njia bora ya yeye kujirudi na kuomba radhi kwa kitendo kile, au ilikuwa ni njia ya kuonesha Wahariri na waandishi wa habari katika umoja wao, hawaungi mkono kitendo cha kuvamiwa kwa kituo cha habari.

Lakini sasa tujiulize, Rais kuwataka Ruge na Makonda wapatane, msimamo wa Jukwaa la Wahariri Tanzania unakuwa upande gani. Chombo hiki maalum kwa ajili ya kutetea maslahi ya waandishi wa habari kimeachwa katika hali gani?

Mbali na TEF, vyombo vingine vya habari kwa kuchukizwa na kitendo hicho, vilisitisha kurusha habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini baada ya kilichotokea mwishoni mwa juma, vyombo hivi vinaendelea na msimamo upi? Endapo wewe ulimchukia mtu kwa vile alimpiga rafiki yako, waliopigana wakipatana, wewe utabaki na chuki au utamsamehe aliyempiga rafiki yako?

Kama ilivyo kwa vyombo vya habari vilivyoachwa njia panda visijue cha kufanywa, ndivyo vivyo hivyo ilivyo kwa maelfu ya wananchi na wanaharakati wa haki za binadamu na walivyoachwa njia panda bila kujua msimamo wao ni upi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kililaani kitendo cha kuvamiwa kwa Clouds Media Group huku waandishi wa habari wakitishiwa kutajwa katika orodha ya watumiaji wa dawa za kulevya. Taasisi hii na nyingine zilizotaka hatua sahihi zichukuliwe ili wahusika waadhibiwe kuweza kuzuia vitendo kama hivi wakati mwingine, vimeachwa katika hali gani?

Ieleweke kwamba, hakuna mtu aliyetaka mgogoro huu baina ya pande hizo mbili uendelee. Kuendelea kwake hakutoi mazingira mazuri kwa ukuaji wa sanaa kwa namna moja, lakini pia wananchi nao walikuwa wanakosa baadhi ya taarifa kutoka kwa kiongozi wao wa mkoa kwa upande mwingine.

Lakini wengi walitaka jambo hili limalizwe katika njia ambayo pande zote zingeriadhia na bila kuacha manung’uniko ya huyu kuona hakutendewa sawa.

Kwa ushahidi wa kimazingira, ni dhahiri kuwa mgogoro huo umekwisha na kama haujaisha basi kwa sasa hauna kichwa wala miguu, lakini swali moja linalobaki ni, Je! Wahusika wameriadhia kwa mioyo yao kuyamaliza au kwa sababu ametakiwa kufanya hivyo na Rais. Na ujue, huwezi kukataa ombi la Rais, kwani kiuhalisia hakuombi, anakuagiza!

Utatuzi huu unatoa nafasi ya tatizo kujirudia au kutojirudia?
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Utashi, ni kitu kikubwa sana katika uongozi. Hakuna shortcut. Hii ieleweke. Uongozi unahitaji umakini sana na si kukurupuka. Pia kuelewa kwa watu, kunawanaoelewa (kufundishika) kuna hata ufanyeje, uelewaji wa mtu binafsi ni kipaji kikubwa si kila mtu anacho. Tunao viongozi wengi sana barani Africa na Duniani, Ni wachache sana wenye kipaji cha kujielewa cha hali ya juu.Viongozi wachache waliopita ambao walikuwa na kipaji hiki, Raisi wa kwanza wa Botswana, Raisi Kwame nkuruma, Ghana, Raisi wa kwanza Senegal, Na Mheshimiwa sana Raisi Nyerere.Pia Patrice Lumumba wa congo, aliuwa akiwa kijana mdogo, Mabepari walimtoa ili waingilie njia zote kuu za uchumi Congo. Mpaka leo Congo ipo njia panda. Maraisi wengi waliotawala Africa, wamekosa sifa, wameirudisha Africa kulkule tulikotoka kwenye mikono ya Wanyama. Watanzania wengi mmejisahau. Wengi bado mnaunga mkono ubepari unaotula sababu tu wavivu wa kufikiri, na tu wavivu wa kutumia akili, na tumekosa uhodari.Tunalaumu, lakini tunachangia sisi wenyewe udhalimu huu. Tunaukubali, ingawa tunapiga kelele.Ni kelele tupu.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad