Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Abdulkarim Hamis Mruma kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Emmanuel Buhohela uteuzi wa kiongozi huyo umeanza tarehe 17 Agosti, 2017.
Wengi watamkumbukwa Profesa Mruma kwa umaarufu wake aliojizolea wakati akiongoza kamati ya wataalamu waliofanya uchunguzi kwa lengo la kubaini kiwango cha madini kilichokuwemo katika makontena yenye mchanga wa madini yanayoshikiliwa maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kamati hiyo iliyoteuliwa Machi 29 mwaka wakati wa kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wake ilisema kwamba imebaini mambo mengi ikiwa ni pamoja na uwepo wa dhahabu kiasi kikubwa kwenye makinikia. Katika makontena 277 yaliyozuiliwa kulikuwa na tani saba za dhahabu yenye thamani zaidi ya shilingi Trilioni moja nukta moja nne saba.
Aidha, katika uchunguzi hiyo Kamati ilibaini uwepo wa madini ya shaba, fedha , sulphur pamoja na chuma ambayo yote kwa pamoja hayakuwa yakibainishwa wakati wa usafirishaji mchanga.
Kabla ya uteuzi huo mpya wa Agosti 17, Prof. Abdulkarim Hamis Mruma alikuwa ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania.