Hatimaye utata uliokuwa umeenea wa kuwepo kwa ufujaji na matumizi mabaya ya fedha kiasi cha milioni 285.49 zilizokuwa zimechangwa na wadau pamoja na serikali kwa ajili ya rambi rambi ya vifo vya ajali ya basi la wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent umekwisha baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kukabidhi milioni 23.27 kwa wazazi wa watoto walionusurika katika ajali hiyo.
Akikabidhi fedha hizo mbele ya waandishi wa habari ambapo kila mzazi alipata Tsh. Milioni 7.75, Gambo alisema fedha hizo zilikuwa zimebaki baada ya matumizi ya shughuli za mazishi kwa watoto 32 walimu wawili na dereva waliokuwa wamekufa katika ajali hiyo na matumizi mengine yakiwemo ya wazazi waliokuwa nchini marekani kwa ajili ya kuwauguza watoto wao na kwamba matumizi ya fedha hizo watapanga wao wenyewe.
Katika hatua nyingine Gambo alisema Serikali imekubali kutoa wataam wa saikolojia kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia watoto walionusurika katika ajali ya basi la wanafunzi ili kuwaweka sawa na pia kuwaandaa kufanya mtihani wa darasa la saba unaowakabili mnamo mwezi Septemba.
Aidha Gambo alisema kazi ya kutoa tiba ya kisaikolojia pia ilishafanyika kwa wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent. Wakizungumza baada ya kukabidhiwa fedha hizo wazazi wa watoto hao wameishukuru serikali na wafadhili kutoka marekani kwa msaada mkubwa kwa watoto wao tangu mwanzo hadi sasa.
Mhe Gambo katika picha ya pamoja na manusura wa ajali ya Lucky Vincent walipotembelea ofisi yake mapema hii leo.
Aidha wazazi hao walisema pamoja na watoto wao kuwa nje ya shule kwa zaidi ya miezi mitatu wako tayari kufanya mtihani na kumaliza elimu ya msingi unaotarajiwa kufanyika mwezi September.
RC Gambo akiwakabidhi wazazi wa Doreen Mshana jumla ya Shilingi Milioni 7.75 ikiwa ni bakaa ya michango ya rambirambi.
Kwa mujibu wa Gambo, baada ya kutokea kwa ajali hiyo mwezi Mei 2017, wadau mbalimbali na serikali walijitolea na kuchanga fedha na kupatikana zaidi ya milioni 285.49 ambazo nbaada ya matumizi zilibaki milioni 23.27 ambazo zilikabidhiwa jana.
Gambo Amaliza Utata wa Rambi Rambi za Ajari ya Watoto Lucky Vincent
0
August 23, 2017
Tags