Mwenyekiti wa mfuko wa Graca Machel, Graca Machel amewataka wanawake kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi za Afrika.
Akizungumza leo Jumamosi wakati wa kufunga mkutano wa siku nne wa kuwaendeleza wanawake kiuchumi na kijamii, Machel alisema wanawake wengi wamekuwa wakifanya shughuli zao nyuma ya pazia na kutegemea msaada wa wengine.
Alisema walio wengi wanaweza kujisimamia wenyewe kutokana na kufanya vitu vingi, lakini wanaogopa kufanya hivyo kwa kusikiliza nafsi inayowakatisha tamaa.
" Mnaweza, kuweni sehemu na chachu ya mafanikio, fikirieni vitu vikubwa, kuweni mabalozi wa wasiolisikia hili" alisema Machel.
Kwa upande wake Evelyne Warioba ambaye ni mke wa waziri mkuu mstaafu Joseph Warioba alisema mbali na kujenga uhusiano, kukutana na wanawake wengi wa Afrika, alichojifunza na anachokwenda kufanya ni kuhakikisha wanawake wanafikiwa popote pale walipo.
Alisema hatua ya kwanza kabla ya kupiga mwendo ni kuhakikisha wanawake wanashikana mkono na kwenda pamoja.
" Tuwafikie, tuwaeleze, wajue kuwa wao ni sehemu ya maendeleo ya nchi na Afrika kwa ujumla," alisema Warioba.