INASIKITISHA sana! Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkamba Kata ya Kimanzichana mkoani Pwani aliyetambuliwa kwa jina moja la shabani anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 50, anadaiwa kufia kifuani mwa binti mwenye umri wa chini ya miaka 30, wakiwa kwenye gesti moja iliyopo Mzinga-Mbagala jijini Dar.
IJUMAA WIKIENDA LATONYWA
Mara tu baada ya kujiri kwa tukio hilo lililoibua simanzi nzito, Ijumaa Wikienda ambalo huwa halilazi damu kufika eneo la tukio na kuanika kila kitu, lilitonywa na chanzo chake, mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo lilifika na kuibuka na mkanda kamili wa sakata hilo. Wawili hao walidaiwa kufika kwenye gesti hiyo na kuomba huduma ya kulala kabla ya kutokea kwa tukio hilo baya.
WALITOKEA KIMANZICHANA
Mwenyekiti huyo alikumbwa na umauti Agosti 11, mwaka huu ambapo kwa mujibu wa meneja wa gesti hiyo, Hamadi Haji, walipofika, wawili hao walichukua chumba tangu Agosti 8, mwaka huu wakitokea huko Kimanzichana. Meneja huyo aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, baada ya kulipia chumba, wawili hao walikuwa wakifika usiku kulala na mchana walikuwa wakitoka kwenda kwenye mihangaiko yao. “Sijui walikokuwa wakienda, lakini walikuwa wakirudi usiku na kujifungia chumbani.
MSHANGAO
“Lakini katika hali ya kushangaza leo (Ijumaa iliyopita) asubuhi, mwanamke aliyekuwa na mwenyekiti alinifuata na kuniambia mwenzake huyo hamwelewi kwa sababu ghafla alianza kumbadilikia na kukoroma kwa mlio ambao haukuwa wa kawaida.
“Yule mwanamke aliniambia kiongozi huyo alikuwa na dozi fulani aliyopewa baada ya kutoka hospitalini kwa sababu hakuwa vizuri kiafya na hilo ndilo lililowaleta Dar. “Alisema alimkatalia sana wasifanye tendo la ndoa, lakini usiku mzima alikuwa akimlazimisha. “Yule mwanamke alitueleza kuwa baada ya jamaa kumbembeleza sana na kumuongezea na vishawishi vingine, mwanamke alisema alijikuta akilegeza msimamo kisha akamkubalia asije akaona labda hampendi. “Baada ya kumkubalia ndipo wakaanza kufanya yao.
.
MUUNGURUMO WA AJABU
“Aliendelea kutusimulia kuwa wakati wakiendelea kufanya yao ndipo alipoanza kumsikia mwenzake akitoa muungurumo wa ajabu huku akimng’angania kifuani. “Alitusimulia kuwa alipoona hivyo, akaanza kumshangaa, lakini ghafla alimuona akitupatupa miguu na mikono.
“Alisema baada ya kuona hivyo, alijinasua na kumwangalia mwenzake kwa makini ndipo akamshuhudia akitupatupa mikono na miguu peke yake. “Yule binti alisema kila alipojaribu kumsemesha, jamaa alikuwa hawezi kujibu lolote hivyo alikaa muda fulani akijua mwenzake labda amekumbwa na jambo la kawaida na atarejea kwenye hali yake.
UKIMYA WATAWALA
“Alisema tofauti na matarajio yake, jamaa aliendelea kuwa kimya na hapo ndipo alipoingiwa na hofu. “Alipoona hivyo, ndiyo akaja kunigongea kwenye ofisi yangu. Mimi nikaenda naye kwenye chumba chao kiitwacho Mikumi na kumkuta jamaa amelala kwa staili ambayo hata mimi mwenyewe sikuilewa.
“Ilibidi nimpigie simu mwenyekiti wa serikali ya mtaa wetu, aje tushirikiane kumuangalia,” alisimulia meneja wa gesti hiyo na kuongeza: “Muda mfupi baadaye, mwenyekiti aliwasili na viongozi wenzake na kuingia kwenye hicho chumba ambapo walipomuangalia jamaa, waliniambia kuwa huenda amefariki dunia. “Hapo ndipo wakapiga simu polisi ambao walifika na kuuchukua mwili huo baada ya kugundua jamaa alikuwa amekwishafariki dunia.”
Kufuatia sakata hilo, Ijumaa Wikienda lilifika kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mzinga A na kumkuta mwenyekiti wa mtaa huo, Chande Mpwati ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo mtaani kwake na kueleza jinsi alivyoshiriki katika kwenda kuukagua mwili wa marehemu na kumuhoji binti aliyekuwa naye.
MAPENZI YA SIRI
Mpwati alisema kuwa, alipomuhoji binti huyo alimwambia kwamba jamaa huyo alikuwa ni mpenzi wake wa siri kwa kuwa ana familia yake kijijini kwao, Mkamba maana mwanamke huyo naye ni mkazi wa huko hivyo walikuja Dar kwa ajili ya mwanaume huyo kutibiwa ambapo walinionesha makaratasi ya hospitalini ndipo umauti ukamfika wakiwa wanafanya mapenzi. “Mwili wake ulichukuliwa na polisi kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Temeke na yule binti alichukuliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema mwenyekiti huyo.
KAMANDA TEMEKE
Ijumaa Wikienda lilizungumza na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, ACP Gilles Muroto ambaye alisema kuwa ishu hiyo ilikuwa haijamfikia mezani kwake, lakini aliahidi kufuatilia kwa watu walio chini yake.