Jakaya Kikwete: Wanasiasa wa Upinzani Wasichukuliwe na Serikali kuwa ni Maadui

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea umuhimu wa utawala bora na kuheshimu sheria, akitaka Serikali barani Afrika zisichukulie vyama vya upinzani kuwa ni maadui.

Kikwete pia amesema wanasiasa wa upinzani wasichukuliwe na Serikali kuwa ni maadui, huku akiwashauri wabunge wa vyama tawala barani Afrika kuzikosoa Serikali zao wanapoona zinakwenda kinyume na ilani ya uchaguzi.

Akijadili mada iliyowasilishwa juzi na Barney Pityana, ambaye ni makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kuhusu Utawala Bora na Sheria, Kikwete alitaka vyama vya kisiasa barani Afrika kuishi kwa amani.

Kikwete, ambaye kwa sasa anasifiwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwa kuheshimu demokrasia, alisema vyama vya kisiasa vilivyo madarakani havitakiwi kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui bali wabia katika kuendeleza misingi ya demokrasia kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Nne ambaye amekuwa nguzo muhimu katika kurejesha amani nchini Libya, aliwakumbusha washiriki katika mkutano wa Jukwaa la Uongozi Barani Afrika kuwa vyama vingi barani Afrika bado vinakua.

Akitoa mfano wa Tanzania, Kikwete alisema siasa za vyama vingi zilirejeshwa mwaka 1992 na bado vinajijenga ili wananchi waelewe sera zao.

Aliwataka wabunge kutoka chama tawala kuiwajibisha Serikali wanapoona wizara hazifanyi kazi kama ilani inavyotaka.

"Ni kitu kizuri kwa wabunge kama hawa kuhoji pale kunapokuwepo na mgogoro katika sehemu moja barani Afrika, na hili ni jambo muhimu kunapokuwepo na utawala wa sheria unaozaa utawala bora".

Pia, Kikwete alitaka vyama vya upinzani kukubali kushindwa baada ya uchaguzi kufanyika kwa haki, uhuru na Kidemokrasi.

Kwa mujibu wa Kikwete, utawala bora bila ya kuwa na serikali imara hauwezekani, kwa hivyo akasema huna haja ya kuwa na Bunge imara ambalo litaihoji serikali wakati itakapoonekana muhimu kufanya hivyo.

Akizungumzia haja ya kuendeleza amani na usalama, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alivitaka vyombo vya habari kuwa na uzalendo wakati vikitoa huduma kwa ajili ya kuboresha bara la Afrika.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki aliwataka viongozi wa Afrika kustawisha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanalindwa.

Viongozi watano wa zamani wa nchi za Afrika, ambao ni Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Mkapa na Kikwete (Tanzania), Bakili Muluzi (Malawi) na Mbeki wanahudhuria mkutano huo unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini.

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad